Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFISA MTENDAJI AUAWA KWA KUBANWA PUMZI MBEYA

Mwili wa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kabwe, katika kata ya Iyela jijini Mbeya Clementine Enock (34) umekutwa ukiwa umetelekezwa katika eneo la Airport ya zamani baada ya kuuawa na watu wasiofahamika kwa kubanwa pumzi.


Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa walibaini kuwepo kwa mwili huo Januari mbili, mwaka huu majira ya saa moja asubuhi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.


Kidavashari alifafanua kuwa kabla ya tukio hilo marehemu aliondoka nyumbani kwao siku ya Mwaka mpya na kuaga kuwa anakwenda Airport kwenye sherehe ya rafiki yake huku akiwa na gari yenye namba za usajili T234 DJM aina ya Toyota Spacio.


Alisema kuwa ndugu wa marehemu walipata hofu mara baada ya ndugu yao kuchelewa kurudi nyumbani na ndipo wakaanza kumpigia simu bila mafanikio mpaka usiku wa manane.


“Marehemu aliaga nyumbani kwao Uyole ya Kati alikokuwa akiishi majira ya saa kumi jioni siku ya tarehe moja kwa madai anaenda kwenye sherehe ya rafiki yake akiwa na usafiri wa gari lake, ambapo mpaka kufika usiku wa manane hakukuwa na taarifa yeyote ndipo hofu ikatanda kwa familia ambapo walipiga simu kwa ndugu jamaa na marafiki na kueleza kuwa hawajui alipo,” alisema Kidavashari.



Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari siku iliyofuata majira ya saa moja asubuhi mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo la wazi jirani na Shule ya Sekondari ya Samora ambapo uchunguzi wa awali unaonesha kifo chake kilitokana na kubanwa pumzi na watu wasiofahamika.


Alisema mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa marehemu aliuawa na mtu wa karibu yake huku akisema tukio hilo lilifanywa ndani ya nyumba ya mtu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com