Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia binti aliyejulikana kwa jina la Neema Japhet (23) kwa tuhuma ya kumtupa mtoto wa siku moja kwenye choo cha kanisa la Afrika Inland Church Tanzania (AICT) la Kitangiri katika manispaa ya Shinyanga.
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa Elias Mwita alisema mwanamke huyo alikamatwa Januari 24,2017 majira ya saa tatu asubuhi na majirani zake chumbani kwake alipokuwa amepanga eneo la Kitangiri na kisha kutoa taarifa polisi .
Mwita alisema jeshi la polisi lilifika katika eneo hilo kisha kumkamata kwa tuhuma ya kumtupa mtoto wa siku moja chooni baada ya kujifungua siku ya Ijumaa wiki iliyopita na baada ya kuhojiwa alikiri kufanya kitendo hicho.
“Baada ya mtu aliyetupa mtoto huyo kutojulikan, tulitoa wito kwa wananchi ili kushirikiana nasi ili kumbaini na juhudi za wananchi za kumsaka zimezaa matunda sasa majirani wameweza kumbaini mwanamke huyo kuwa ndiye aliyehusika na unyama huo na amekiri kuhusika na utupaji wa mtoto”,alisema Mwita.
Mwita alieleza kuwa mwanamke huyo alidai alikwenda chooni kwa lengo la kujisaidia lakini ikatokea bahati mbaya mtoto atumbukia kwenye tundu la choo.
Aliongeza kuwa hivi sasa wanafanya utaratibu wa sheria ili kumfikisha mahakamani ili kujibu tuhuma hiyo.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kitangiri Habiba alisema mtoto huyo alitupwa chooni mnamo majira ya saa kumi na moja jioni tarehe 20/01/2017 ambapo baadhi ya waumini wa kanisa hilo walisikia sauti ya mtoto mchanga ikitokea katika choo cha kanisa.
Jumanne alisema walichukua jukumu la kubomoa choo hicho na kumkuta mtoto akiwa hai kisha kumpeleka katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga ingawa hata hivyo mtoto huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog