Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania ( THRDC) leo Jumatano ya Januari 11, 2017 wamefungua kesi ya kuipinga Sheria Mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12 ya mwaka 2016 katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kesi hiyo, Katibu Mtendaji MCT, Kajubi Mukajanga amesema washirika waliofungua kesi hiyo wanataka baadhi ya vifungu vya sheria vinavyokandamiza uhuru wa habari na kujieleza vifutwe kwakuwa vinakiuka matakwa ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Na kwamba mahakama ya EACJ imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huo na kuhakikisha nchi wanachama wanaufuata na kuusimamia.
“Vifungu hivyo vya sheria vinakandamiza uhuru wa habari na wa kujieleza, vifutwe kwani vinakiuka matakwa ya mkataba wa EAC ambao unataka nchi mwanachama kuzingatia na kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye ibara ya 6(d) na 7(2),”amesema.
Amesema kuwa, Ibara ya 6(d) ya mkataba wa EAC inahimiza umuhimu wa kufuata kanuni za utawala bora, wa kidemokrasia, sheria, uwajibikaji, uwazi na haki kwa wote ikiwa pamoja na usawa wa kijinsia, kulinda na kuheshimu haki za binadamu.
“Kama ilivyo kwenye kifungu cha 8(1) (c), Tanzania inatakiwa kuchukua hatua za kuhakikisha haki zote zinazotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na kutekelezwa,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba amesema baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakiuka haki za binadamu na kwamba wameshiriki kufungua kesi hiyo ili kuipinga sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
“Sheria imekaa sivyo, tumeona tuungane na wenzetu ili kuipinga sheria hii,” amesema.
Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema sheria inabidi ibadilishwe hasa katika vifungu kandamizi kabla ya kuanza kutumika.
“Kuna mazingira yatakayowaweka katika mazingira magumu waandishi wa habari, ni vyema kuipinga sheria hii isitumike hadi ibadilishwe.”