Bibi mwenye umri wa miaka 60 amekutwa amekufa mkoani Tabora huku amevaa nguo nyeusi aina ya kaniki, akiwa na vibuyu vitano na kuku mweupe, katika mazingira yanayoashiria kushiriki vitendo vya kishirikina.
Aidha, mwili wa mtu mwingine umekutwa pembeni ya mti aliokuwa akichimba dawa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Selemani iliwataja waliokutwa wamekufa kuwa ni Nsoma Dotto (60) mkazi wa Kijiji cha Zugimlole Wilaya ya Kaliua na Mayara Marashi (50) ambaye ni mkazi wa Igunga.
Kamanda Selemani alisema Nsoma alikutwa akiwa amekufa umbali wa mita 200 kutoka nyumbani kwake juzi.
Alisema bibi huyo alikutwa amevaa nguo nyeusi aina ya kaniki akiwa na vibuyu vitano huku pembeni yake kukiwa na kuku mweupe. Uchunguzi wa awali wa jeshi hilo, unaonesha kuwa huenda ni imani za kishirikina.
Aidha, alisema Marashi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mwakapinga, Kata ya Nanga, aliyekuwa mganga wa kienyeji, mwili wake uliokotwa Januari 16, mwaka huu ukiwa umeanza kuharibika.
Kwa mujibu wa Kamanda Selemani, mganga huyo wa kienyeji aliondoka nyumbani kwake Januari 8, mwaka huu kwenda porini kuchimba dawa, lakini hakurudi kijijini hadi maiti yake ilipookotwa akiwa amekufa.
Alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho. Aliwaomba wananchi wanaoenda porini kwa ajili ya shughuli zozote zile, wawe wanatoa taarifa kwa ndugu zao ili iwe rahisi tatizo linapotokea.
Social Plugin