Mwenyekiti was CCM wilaya ya Mbeya mjini ndugu Ephrahim Mwaitenda akifikishwa hospitali ya Rufaa mkoa wa Mbeya asubuhi ya leo Jumatatu Januari 30,2017,Kulia ni kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya ndugu Lobe Zongo akimpokea Mwaitenda katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mbeya baada ya kudaiwa kupigwa risasi.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Mbeya mjini, Ephreim Mwaitenda amenusurika kifo baada ya watu wasiofahamika kumvamia shambani kwake wilayani Kyela akiwa amelala usiku na kumjeruhi kwa risasi mgongoni.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Emmanuel Lukula amesema Mwaitenda alipigwa risasi baada ya watu hao kuvunja dirisha usiku na kuchana nyavu za dirisha kisha kupenyeza mtutu na kumpata Mwaitenda mgongoni
Lukula alisema baada ya kufyatua risasi watu hao walitokomea
kusikojulikana ambapo Mwaitenda alidhani kuwa ni simu imepasuka lakini alitahamaki akivuja damu mgongoni.
Kaimu Kamanda Likula alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa nane usiku ambapo Mwenyekiti alitoa taarifa kituo cha Polisi Kyela.
Alisema askari walifika eneo la tukio na kumchukua majeruhi hadi
hospitali ya Wilaya ya Kyela na kufanikiwa kuondoa baadhi ya risasi zilizotengenezwa kwa goroli na ambazo zimetumiwa na bunduki iliyotengenezwa kienyeji.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Lobe Zongo alisema majeruhi amefikishwa hospitali ya rufaa Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi.
Aidha Katibu Zongo amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufika haraka eneo la tukio pamoja na Madaktari ambao wanafanya juhudi za kuondoa risasi zilizokwama mgongoni.
Kaimu Kamanda Lukula alisema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watu waliofanya uhalifu huo walidondosha baadhi ya vitu ambapo wanavifanyia kazi.
Aidha baadhi ya wananchi Mkoa wa Mbeya na Wanasiasa wanalihusisha tukio hilo na siasa kutokana na mwaka huu ni Uchaguzi wa Vyama vya siasa.
“Lazima waliofanya hivyo ni wagombea wa nafasi Fulani ndani ya Chama na walitaka kummalizi ili waweze kupita kirahisi lakini tusubiri ripoti ya Jeshi la Polisi tuone wahusika wenyewe” alisema mmoja wawananchi wa sharti la kuhifadhi jina lake.
Chanzo- Mbeya yetu blog