DAKTARI BINGWA : UGUMBA UNAWATESA WANAUME WENGI ZAIDI KULIKO WANAWAKE

IMEELEZWA kuwa matatizo ya uzazi yapo zaidi kwa wanaume kuliko kwa wanawake tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi.

Daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake ambaye pia alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Udaktari kabla ya kuwa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), ambaye hivi sasa ni mstaafu, Profesa Malise Kaisi alisema hayo katika mahojiano maalum na HabariLeo, jijini Dar es Salaam.

Profesa Kaisi alifafanua kuwa, mara nyingi wanawake aliowafanyia tiba ya matatizo ya ugumba ni wale ambao waume zao walikuwa na kasoro katika uwezo wao wa kuzaa na si wao. “Hapa nina maana kuwa mara nyingi watu tuliowafanyia tiba hii ni wale ambao waume zao walikuwa na kasoro katika uwezo wao wa kuzaa.

“Ushauri katika matatizo ya uzazi ni lazima watu wote wahusishwe si wanawake pekee. Uchunguzi tulioufanya Muhimbili ulionesha kuwa katika kila ndoa 10 zenye matatizo ya uzazi, ndoa nne tatizo lilikuwa kwa mwanamke na nne tatizo lilikuwa kwa mwanamme. Ndoa mbili zilizobaki tatizo lilikuwa pande zote, lakini zaidi kwa wanaume, kuliko wanawake,” alisema.

Alisema mawazo yaliyojengeka kwa watu wengi kuwa matatizo ya uzazi yapo kwa wanawake pekee si sahihi kwani katika tiba ya namna hiyo inashauriwa wanandoa wote wafike kwa daktari na si mwanamke peke yake.

Dk Kaisi alisema mahusiano yasiyokuwa ya karibu katika ndoa yamewafanya kwa kiwango kikubwa wanandoa wengi kutokupata watoto na hivyo kuingiwa na hofu kuwa wana matatizo ya uzazi.

Akifafanua hilo alitoa mfano kwa ndoa moja kuwa kwa miaka saba tangu walipooana walikuwa hawajapata watoto hivyo alipozungumza nao akabaini kuwa kazi wanazozifanya zimesababisha wawe mbali muda mwingi.

“Unakuta baba kazi yake ni kusafiri kila mara na mama naye hivyo, siku wanapokutana inakuwa si siku sahihi kwao, matokeo yake wanalalamika kuwa hawapati watoto kumbe ni elimu tu inatakiwa hapo.Baada ya kukutana na wanandoa hao na kuwashauri haikupita muda wakapata watoto,” alisema.

“Tatizo la elimu limekuwa ni sababu kubwa ya wanandoa kutoshika mimba. Maisha ya sasa watu wapo mbiombio kutafuta fedha hivyo hawajui siku sahihi za wao wanazostahili kukutana na kupata mtoto. Inawezekana hicho nacho ni kisababishi.”

Alitaja sababu nyingine zinazoweza kuchangia wanandoa kutopata watoto kuwa ni chuki na mifarakano katika ndoa. Matatizo ya uzazi kwa wanawake Akina mama wana matatizo mengi, mojawapo kubwa linalowasumbua ni tatizo la kutokushika ujauzito.

Mwanamke kushindwa kupata ujauzito kwa kipindi cha ndani ya mwaka mmoja au zaidi ya mwaka mmoja wakati mwanaume na mwanamke wanakutana kwa muda unaotakiwa na bila kutumia njia za kuzuia mimba ni tatizo.

Kuna aina mbili ya tatizo hili moja hujulikana zaidi kwa jina la primary infertility. Hii humaanisha kuwa mwanamke hajawahi kushika ujauzito maishani mwake.

Pili ni secondary infertility, hii humaanisha kuwa aliwahi kupata mimba lakini ikashindikana kupata nyingine, na ya tatu ambayo hutokea mara chache kama asilimia 20 hujulikana kama fecundability ambapo mwanamke anakuwa na uwezekano wa kupata mimba ndani ya mzunguko mmoja wa hedhi.

Matatizo ya uzazi kwa wanaume Ugumba kwa mwanaume, ni hali ambayo mwanaume anashindwa kumpa mimba mwanamke, tatizo hili kwa mujibu wa takwimu zilizopo huwaathiri wanaume kwa asilimia 40 hadi 50 na huwapata takriban asilimia saba ya wanaume.

Ugumba kwa wanaume kwa kiasi kikubwa husababishwa na tatizo katika uzalishaji na utoaji wa mbegu za uzazi.

“Tunaposema mwanaume ni mgumba ni pale ameishi na mwanamke kwa mwaka mmoja na tendo la kujamiiana linaendelea kikamilifu lakini hatuoni matokeo. Ingawa tatizo la uzazi lipo pande zote mbili kwa mwanamke na mwanaume, lakini mwanaume pia ana asilimia kubwa ya kuwa na tatizo la uzazi kama ambavyo tumekwishaona hapo awali.”

Tatizo la uzazi linatokea kwa mtu yeyote bila kujali kama alishawahi kumpa mimba mwanamke au kama ni mwanamke pia haijalishi kama alishawahi kupata ujauzito siku za nyuma.

Mtu anaweza kuwa na historia nzuri kuwa alishawahi kumpa mimba mwanamke lakini linaweza kutokea tatizo akashindwa kusababisha ujauzito tena.

Chanzo mojawapo katika sehemu hii ni matumizi ya baadhi ya madawa yawe ya hospitali, ya asili au ya kulevya ambayo huathiri kwa kiasi kikubwa uzazi na ndiyo maana inashauriwa unapokuwa na tatizo muone daktari kwa uchunguzi zaidi na tiba.

Walevi nao huathirika sana na matatizo ya uzazi kwani ulevi wa kupindukia huathiri utendaji wa tendo la kujamiiana na uzalishaji wa mbegu za kiume. Kuendesha baiskeli mwendo mrefu na kwa muda mrefu pia ni mojawapo ya vyanzo.

Matatizo ya vinasaba nayo huchangia. Uvutaji wa sigara kwa mwanaume unaathiri uzalishaji wa mbegu za uzazi kwa asilimia thelathini, kemikali zilizomo kwenye tumbaku zimethibitishwa kuua mbegu za kiume ndiyo maana pamoja na madhara mengi ya sigara ndiyo maana makampuni yanayotengeneza sigara huweka onyo kwa wavutaji wa sigara kwamba ni hatari kwa maisha yao.

Aidha aina ya mavazi yanayovaliwa na wanaume yanaweza kusabnabisha kiwanda cha kutengeneza manii kuvia. Kiasili kiwanda cha kutengeneza manii hutakiwa kuwa na joto la wastani na kutobanwa kwa muda mrefu.

IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI-HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post