DK POSSI: NIMEJIUZULU UBUNGE...HIVI KWELI MNADHANI NITAKUWA NI MROHO KIASI GANI


NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu, Dk. Abdallah Possi, amesema tayari amemwandikia barua ya kujiuzulu ubunge Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutokana na hatua ya Rais Dk. John Magufuli kumteua kuwa Balozi.

Dk. Possi ambaye alikuwa miongoni mwa wateule wa ubunge wa Rais John Magufuli, uamuzi wake huo ni wazi unavunja mjadala dhidi ya Mkuu huyo wa nchi aliyekuwa akikabiliwa na madai ya kwenda kinyume na Katiba kutokana na uteuzi wake wa wabunge wengine wawili alioufanya wiki hii kuonekana kushindwa kukidhi matakwa ya Katiba katika suala la jinsia.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Dk. Possi ambaye alikuwa mteule wa mwanzo katika Serikali ya Rais Magufuli kabla ya juzi kutangaza kumteua kuwa balozi alisema baada ya taarifa hiyo ya Rais jana alimwandikia barua ya kujiuzulu ubunge Spika wa Bunge.

Mahojiano kati ya gazeti hili na Dk. Possi ambaye kwa sasa anasubiri kupangiwa kituo kipya cha kazi yalikuwa kama ifuatavyo:-

Swali: Dk. Possi hongera sana, umejisikiaje Mheshimwa Rais kukuteua kuwa balozi?

Dk. Possi: Ni kazi nyingine mpya, majukumu tofauti ni challenge (changamoto) nyingine kwa sababu nakwenda kuwa mwakilishi katika nchi nyingine.

Kwa hiyo ni kuichukua hiyo changamoto kwa jinsi inavyokuja kwa manufaa ya Taifa.

Swali: Sasa kwa uteuzi huo wa ubalozi utakuwa tayari kujiuzulu ubunge?

Dk. Possi: Hilo swali nimeulizwa na watu wengi kweli na mimi nikasema hebu ngoja niwape challenge, hivi kweli mnadhani nitakuwa ni mroho kiasi gani, mnajua niko nje halafu mseme sijiuzulu ubunge wakati siwezi kupractize eeeh! Umenielewa?

Swali: Kwa hiyo utajiuzulu?

Dk. Possi: Of course definitely (hakika) kwa sababu haiwezekani uko mbali unawezaje ku- practise ni jibu ambalo liko wazi hata sijui kwanini limekuwa mjadala mkubwa hivyo.

Swali: Kwa hiyo umeandika barua ya kujiuzulu?

Dk. Possi: Yeah nimeshaandika.

Swali: Umeandika lini Dk?

Dk. Possi: Si leo kwa sababu siwezi kuandika kabla ya taarifa

Swali: Umeandika kwa Rais au kwa Spika wa Bunge?

Dk. Possi: Ubunge ni kwa spika kwa hiyo unamwambia spika nimejiuzulu the less ni procedure (zilizobaki ni taratibu) zingine, the fact is (ukweli ni) ni kwamba huwezi kuendelea kuwa balozi and the same time (na wakati huo huo) ni mbunge sasa ni kwa staili ipi hiyo ni wing tu ya kufikia huko na sidhani kama ni big issue (suala kubwa).

Kujiuzulu huko kwa Dk. Possi katika nafasi ya ubunge ni wazi sasa kunampa nafasi Rais Magufuli kukamilisha takwa la Katiba kupitia kifungu Na 66 1(e) kinachompa mamlaka ya kuteua wabunge 10 na kati ya hao angalau watano wawe ni wanawake.

Kabla Dk. Possi kuteuliwa kuwa Balozi na uteuzi wa wabunge wawili ambao ni Profesa Paramagamba Kabudi na Abdallah Bulembo ambao Rais Magufuli aliufanya mapema wiki hii na hivyo kufanya jumla ya wateule wake hao kutimia wanane kati ya 10, kulikuwa na maoni tofauti wengine wakiwa na mtazamo kuwa tayari idadi ya wanaume ilikuwa ikizidi ile ya wanawake na hivyo kwenda kinyume na Katiba.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alikaririwa na gazeti la MTANZANIA jana akisema Rais Magufuli alikuwa hajavunja sheria.

Dk. Mwakyembe ambaye ni Mwalimu wa Sheria na ambaye alikuwa akizungumza kabla ya uteuzi huu mpya wa Dk. Possi, alisema wanaosema Rais kavunja Katiba wangesubiri amalize nafasi 10 za uteuzi ndiyo waseme.

Wakili kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Judith Kapinga, akinukuu kifungu cha Katiba cha 66 alisema Rais alikwenda kinyume na matakwa hayo.

Dk. Milton Mahanga, aliyewahi kuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuibua mjadala huo.

Katika andiko lake ambalo lilikuwa likisambaa kwenye mitandao ya kijamii siku moja baada ya Rais Magufuli kufanya uteuzi wa wabunge hao wawili, Dk. Mahanga alisema uteuzi huo ulikuwa umevunja Katiba kwa sababu kati ya wabunge wanane waliokuwa tayari wameteuliwa wanaume walikuwa sita na kwa maoni yake alisema walipaswa kuwa watano na wanawake angalau watano.

Ibara ya 66 (1) inayoeleza aina ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sehemu ya (e) inasema; “wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau wabunge watano kati yao wakiwa wanawake.”

Mbali na Dk. Possi na kabla ya uteuzi wa Profesa Kabudi na Bulembo, waliokuwa wameteuliwa na Rais kuwa wabunge ni pamoja na Dk. Phillip Mpango, Balozi Dk. Agustine Mahiga huku wanawake wakiwa ni Profesa Joyce Ndalichako na Dk. Tulia Ackson.

LHRC YATOA TAMKO

Ni katika mjadala huo huo, jana Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), kililazimika kutoa taarifa kwa umma kuhusu uteuzi huo wa wabunge zaidi kikienda mbali na kuzungumzia nafasi nyingine.

Katika taarifa hiyo ambayo ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Hellen Kijo Bisimba, LHRC ilieleza kuwa imetathmini mwenendo wa masuala ya kijinsia katika teuzi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini Tanzania.

“Katika tathmini yetu tumejikita zaidi kuangalia katika muktadha wa haki za binadamu na haki za wanawake kwa kuzingatia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania imeridhia kuhusu usawa wa kijinsia vile vile kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na pia sheria nyinginezo.”

Ilieleza kuwa kikanda, Tanzania ni nchi mwanachama wa Umoja wa nchi za Kusini mwa Afrika na hivyo imeridhia mkataba wa Jinsia na Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol ambapo mkataba huu katika Ibara ya 12 inazitaka nchi wanachama kuhakikisha kuwa katika ngazi zote za maamuzi kuna usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50.

Pia Mkataba wa Afrika wa Haki za Wanawake (Maputo Protocol), unapinga ubaguzi dhidi ya wanawake katika ngazi za maamuzi.

“Kimataifa, Mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) katika Ibara ya 7 inazitaka nchi wanachama wa mkataba huo kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kutunga sera, sheria na kuwa katika ngazi za utekelezaji wa sera na sheria hizo (ngazi za maamuzi).”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya LHRC, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 13 inaeleza jinsi ambavyo Serikali itachukua hatua za makusudi kurekebisha matatizo yaliyo katika jamii ili kuondoa ubaguzi na kwamba katika muktadha huo Katiba imetoa mwongozo katika teuzi mbalimbali, kwa mfano wabunge wateule wa Rais Ibara ya 66 (1) (e).

Mbali na hilo la wabunge wa kuteuliwa katika tathmini yao, Kituo hicho kimesema kimeangalia nyadhifa nyingine za uteuzi unaofanywa na Rais kama mawaziri na manaibu waziri, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa halmashauri bado idadi ya wanawake imekuwa chini sana na hivyo kutokuzingatia ulinganifu wa kijinsia.

“Kwa mfano idadi ya mawaziri wanawake ni 4 tu kati ya 19, kati ya wakuu wa mikoa 26 wanne tu ndio wanawake, kati ya wakuu wa wilaya 134 wanawake ni 25 tu na kati ya wakurugenzi wa halmashauri na wilaya 185 wanawake ni 33 tu.”

Kutokana na hali hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeitaka Serikali na mamlaka nyingine za uteuzi kuzingatia mambo makuu manne.

Kwanza, Sheria na Katiba katika teuzi mbalimbali katika nafasi za uongozi.

Pili, kufuata misingi ya haki za kijinsia kwa mujibu wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Serikali imesaini na kuridhia.



Tatu, kuzingatia usawa wa kijinsia na kuchukua hatua za makusudi (affirmative action) ili kuwa na jamii yenye haki na usawa katika suala la uongozi wa nchi.

Nne, Rais aone uwezekano wakurekebisha hii hali iliyojitokeza ya kukiuka maelekezo ya Katiba.

Na Ratifa Baranyikwa-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post