MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Mfenesini imemhukumu Zubeir Ali Zubeir (26) kwenda jela mwaka baada ya kumtia hatiani ya wizi wa kuku mmoja mwenye thamani ya Sh 15,000.
Akisoma hukumu, Hakimu Ussi Khamis Mjombo wa mahakama hiyo ya Mfenesini, alisema mtuhumiwa atakwenda jela kutumikia adhabu ya mwaka na akitoka atalazimika kulipa fidia ya Sh 15,000 ambapo Sh 5,000 zitaingia katika mfuko wa Serikali na akishindwa kulipa fidia hiyo atalazimika kwenda jela kutumikia adhabu ya miezi sita zaidi.
Awali, Mwendesha mashtaka wa Polisi, Mohamed Mshenga alidai mbele ya hakimu Mjombo wa mahakama hiyo kuwa, Desemba 12 mwaka jana, Zubeir alitenda kosa la wizi wa kuku mmoja mali ya Yussuf Ali Khamis, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Mara baada ya uchunguzi kukamilika kwa upelelezi na upande wa ushahidi kesi hiyo ilianza kusikilizwa tena Januari 17 ambapo mashahidi watatu walitoa ushahidi wao ambao ulimridhisha hakimu Mjombo na kutoa hukumu hiyo.
IMEANDIKWA NA KHATIB SULEIMAN-HABARILEO ZANZIBAR