KESI YA MAPACHA WA KIARABU KUTISHIA KUUA WAANDISHI WA HABARI SINGIDA KUUNGURUMA JANUARI 16


PACHA wenye asili ya kiarabu wanaoshitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Singida kwa kutishia kuua waandishi wa habari mkoani Singida, watasomewa maelezo ya awali Januari 16.

Pacha hao ambao ni wafanyabiashara maarufu mjini hapa, kwa mara ya kwanza, walifikishwa mahakama hapo, Novemba 18 mwaka jana. Washitakiwa hao, Hassan Salehe na Hussein Salehe (47) ni wakazi wa eneo la mji wa zamani katika kata ya Mughanga, Manispaa ya Singida.

Ilidaiwa na Mwanasheria wa Serikali, Ahmed Seif kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo Novemba 07, mwaka jana saa 3:00 asubuhi katika Ofisi za Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Singida (Singpress) zilizopo eneo la Msufini mjini Singida.

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Terrisophia Tesha, Seif alidai kuwa siku ya tukio washitakiwa walikwenda kwenye ofisi hizo na kutoa maneno ya kutishia kuwaua waandishi wa habari wanaoandika habari kuhusiana na tuhuma inayowakabili kwenye kituo cha polisi.

Awali, watuhumiwa hao walifikishwa Polisi kwa tuhuma za kumpiga binti yao waliyedai ana uhusiano wa kimapenzi na kijana 'mswahili' na kuchukua mali yote ya kijana huyo wakidai ameipata kutokana na kuhongwa na binti yao.

Baada ya vyombo vya habari kutangaza taarifa hizo, ndipo pacha hao walipoamua kwenda ofisi za Singpress na kutoa tishio hilo.

Washitakiwa walikana shitaka na wapo nje kwa dhamana.

IMEANDIKWA NA ABBY NKUNGU-HABARILEO SINGIDA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post