Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIWANDA CHA NYAMA CHA AJABU SHINYANGA....HAKIJAWAHI KUCHINJA HATA MFUGO MMOJA TANGU KIANZISHWE 1975

Image result for kiwanda cha nyama shinyanga
Jumuiya tawala za mitaa Tanzania (ALAT) mkoani Shinyanga imesikitishwa na ujenzi wa kiwanda cha nyama kilichopo mkoani Shinyanga kwa kushindwa kufanya kazi ndani ya miaka 41, na kutofanikisha malengo yaliyokusudiwa huku kikiwa kimepoteza mabilioni ya fedha za umma ambazo zimeshindwa kutambuliwa.


Jumuiya hiyo ilifanya ziara juzi kwenye kiwanda hicho cha nyama kilichopo katika manispaa ya Shinyanga ambacho kilijengwa na serikali tangu mwaka 1975, kwa lengo la kuinua uchumi wa wafugaji ,mkoa, taifa na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, lakini hakijawahi kufanya kazi tangu kijengwe.

Akizungumza kwenye kiwanda hicho mwenyekiti wa ALAT mkoani Shinyanga Boniphace Butondo, alisema ni jambo la kusikitisha kwa serikali kupoteza mabilioni ya fedha kwenye kiwanda hicho, halafu wanashindwa kukisimamia na kupoteza matumaini ya wananchi kunufaika nacho.

“Sisi kama ALAT mkoa baada ya kuona kiwanda hiki tumeazimia kuwa serikali iwataifishe wawekezaji waliobinafsishwa tangu mwaka 2007, ambao waliahidi kukiendeleza lakini wameonekana kuwa matapeli, ili wapewe watu ambao wana nia ya kuungana  na serikali ya viwanda ya awamu ya tano ya viwanda”,alisema Butondo.


Aidha kwa upande wake Ofisa mifugo mkoa wa Shinyanga Beda Chamadata alikiri tangu kiwanda kicho kijengwe (1975) na kupewa mwekezaji (2007) hakijawahi kufanya kazi wala kuchinja mfugo wowote, na kubainisha tayari mkoa umeshaandika barua kwa msajiri wa hazina,ili kirudi mikononi mwa serikali.

Hata hivyo Chamadata alisema kutokana na sheria za nchi serikali haiwezi kuendesha biashara, na endapo wakikitaifisha kiwanda hicho, lazima watatafuta mwekezaji ambaye siyo mbabaishaji mwenye kuendana na kasi ya serikali ya  awamu ya tano ya kufufua viwanda.

Nao wajumbe wa ALAT walieleza kusikitishwa kauli ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Ally Nassoro Rufunga kutoa ushuhuda kwenye kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) 2014,kuwa kiwanda hicho kipo tayari kuanza uzalishaji kwani kimeanza uchinjaji na ameshaonja maini kwa niaba yao.

Na Marco Maduhu-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com