KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema mgogoro wa Zanzibar anaamini atakuwa Rais Zanzibar.
Amesema, mgogoro visiwani humo utamalizika endapo viongozi wa vyama vyote va siasa watakaa chini kufanya mazungumzo.
Akizungumza katika mahojiano katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Azam, Maalim Seif alisema jambo la muhimu ni viongozi kukubali Zanzibar kuna tatizo.
Alisema anaamini kama kuna nia njema, maridhiano yanaweza kupatikana Zanzibar na migogoro yote ya kisiasa kumalizika.
“Hii naamini kabisa, kama kuna nia njema, kila upande ukubali Zanzibar kuna tatizo, ukubali kuna haja ya viongozi kupata ufumbuzi wa tatizo na watapata vipi, ni kwa kushirikiana pamoja,” alisema Maalim Seif aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Alisema Serikali iliyopita ya Umoja wa Kitaifa, ilikuwa na mafanikio makubwa na kwamba anavyoona hakuna kitakachorudisha hali ile, kama si kwa vyama kushirikiana.
“Kila upande ukiona unawakilishwa itasaidia kuleta Wazanzibari pamoja,” aliongeza Maalim Seif.
Aidha, Maalim Seif alisema anajua kuna majaribio makubwa yanafanywa kutafuta ufumbuzi, hivyo ufumbuzi ni vema upatikane ili kuridhisha pande zote, na kwamba kuna njia nyingi ya kupata muafaka na hiyo ni pamoja na kufanyika mazungumzo, lakini ni baada ya kila upande kukubali kuwa Zanzibar kuna tatizo.
Akizungumzia kugombea tena nafasi ya urais mwaka 2020, Maalim Seif alisema ni vema kusubiri ili kuona hali ya kisiasa itakapofika wakati huo.
“Tusubiri kwanza wakati wake tuone kama tunafanikiwa au hatufanikiwi kwenye hili, halafu tutafanya maamuzi,” alisema Maalim Seif ingawa baadaye alisema kuwa karibuni anatarajia atakuwa Rais wa Zanzibar.
“Natarajia muda mfupi ujao, Inshaallah nitakuwa Rais wa Zanzibar,” alisema bila kufafanua anawezaje kuwa rais wakati hakushiriki uchaguzi mkuu wa Machi, 2016.
Akizungumzia mgogoro ndani ya CUF, Hamad alisema Msajili wa Vyama vya Siasa aliruhusu upande wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua Sh milioni 369 ambazo ni fedha za ruzuku na kwamba baadaye chama kitashindwa kuzijibia matumizi yake.
Kuhusu hilo, alisema wamemwandikia Msajili, Gavana wa Benki Kuu (BoT) na pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), waangalie hatua ya kuchukua.
Akizungumzia afya yake, alisema anamshukuru Mungu kwamba afya yake ni njema. Hata hivyo alisema tangu aondoke madarakani, amekuwa akijihudumia mwenyewe katika matibabu na si fedha za serikali ikiwa ni pamoja na matibabu nchini India.
IMEANDIKWA NA REGINA KUMBA- HABARILEO