MANUSURA wa ajali ya jahazi namba Z5512 MV Burudani iliyotokea usiku wa kuamkia jana na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 12 na majeruhi zaidi ya 33, wameeleza kuwa chombo hicho kilipigwa na upepo mkali baharini na kukosa mwelekeo kisha kukatika vipande.
“Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake walilazimika kusimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha upepo na baadaye tukaondoka, lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa na wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadaye kikajaa maji na kukatika katikati, “ alisema Emmanuel Mniga, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, mkazi wa mkoa wa Morogoro, ambaye amelazwa katika wodi ya A1 katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Tanga.
Katika ajali hiyo, miili zaidi ya 12 ya baadhi ya abiria waliokufa maji katika jahazi hilo maarufu kwa jina la Sayari, lililokuwa likisafiri kutoka jijini Tanga kwenda mkoa wa Kaskazini Pemba, iliopolewa na imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha hospitali hiyo ya Bombo.
Aidha abiria wengine zaidi ya 33 waliojeruhiwa, wamelazwa katika hospitali hiyo, ambapo wawili kati yao wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi maalumu. Kati ya majeruhi hao, wamo watu wazima sita (6) na watoto sita (6) waliokuwa wakisafiri pamoja na wazazi wao katika chombo hicho, ambacho mpaka jana mchana idadi kamili ya abiria waliokuwemo haijafahamika.
Ilielezwa kuwa baadhi ya wakazi walioliona jahazi hilo kabla ya kuanza safari, walidai lilikuwa limebeba shehena ya mzigo ambao ni bidhaa mbalimbali ikiwemo pumba, maharage, vinywaji aina ya bia na abiria zaidi ya 50 wakiwemo watu wazima pamoja na watoto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha tukio hilo na kusema walipokea taarifa za kupatikana kwa miili ya baadhi ya abiria hao jana saa 12.30 asubuhi na kuanza kufuatilia.
“Ajali ilitokea saa 7.30 usiku wa kuamkia jana na taarifa za awali zinaonesha chanzo cha ajali hiyo ni dhoruba kali,” alisema. Aliongeza, “Tulipata taarifa ya kuzama majini kwa chombo hicho cha mv Burudani maarufu kama Sayari kinachomilikiwa na mkazi mmoja wa Pemba aliyetambulika kwa jina moja la Suleiman maarufu Bwimbwi..... Chombo hicho kilitokea bandari isiyo rasmi (bubu) eneo la Sahare hapa jijini Tanga kuelekea Kaskazini Pemba na ndipo kikakutwa na ajali hiyo, “ alisema.
Kamanda Wakulyamba alisema pamoja na kupatikana majeruhi na miili hiyo, Polisi kwa kushirikiana na majeshi ya Wanamaji, Zimamoto na Uokoaji na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanga bado wanaendeleza jitihada za kutafuta abiria wengine kwasababu idadi yao bado haijajulikana.
“Tatizo lililopo ni kwamba idadi kubwa ya vyombo vinavyosafirisha abiria na mizigo kati ya Tanga na Pemba havina mifumo rasmi ya utambuzi pamoja na ile ya mawasiliano ambayo ingeweza kutumika kurahisisha mawasiliano baina ya walioko chomboni na wenzao walioko nchi kavu wakati wa safari ili kusaidia kufanya mawasiliano hasa wakati inapotokea ajali kama hii, “alisema.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo, Dk Goodluck Mbwilo akizungumza jana mchana katika mahojiano nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo alikiri kupokea miili 12 pamoja na majeruhi 33.
“Majira ya saa nne jana asubuhi ndipo tulianza kupokea maiti pamoja na majeruhi ambao 33 tumewalaza katika wodi zetu za A 1 na A2 wakiendelea na matibabu... na tayari hapa tumeanza kuruhusu wananchi ili waje kutambua marehemu”, alisema.
Kwa upande wake, muuguzi wa zamu katika wodi ya A2, Judith Mzia alimweleza mwandishi kwamba amepokea jumla ya majeruhi 17 kati yao wakiwemo watoto watatu na wanawake watu wazima.
“Majeruhi 15 wanaendeleza vizuri baada ya kupata huduma lakini wawili kati yao hali za afya zao hazijaimarika inaonekana walikunywa maji mengi hivyo wapo katika uangalizi maalumu na hapa kama unavyoona mmoja wao ndio tunajaribu kumwekea hewa ya oksijeni, “ alisema.
Baadhi ya majeruhi wasimulia mkasa Mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, Juma Maduhu ambaye amelazwa wodi ya A1 alisema, “Baada ya kuwasili hapa Tanga tukitokea Bariadi mimi na wenzangu wawili.
Tulianza safari yetu kuelekea Pemba kwa jahazi hiyo saa 5 usiku nikiwa nimeambatana na ndugu zangu, Joji Nindwa na John Kombo na baada ya muda majira ya saa 7.30 usiku, ndipo tulipokumbwa na ajali hii ila namshukuru sana Mungu kwa sababu ndugu zangu wote nimewaona wapo salama, “alisema.
Mariam Idi, mkazi wa Moa wilayani Mkinga, ambaye amelazwa wodi ya A1 alisema katika safari yake hiyo, waliambatana na ndugu zake watano wa familia moja.
“Tulikuwa watu wazima wawili ambapo mwenzangu anaitwa Halima pamoja na watoto wetu watatu sasa ilipofikia saa 7.30 usiku kulikuwa na upepo mkali ambao ulisabisha chombo kuyumba na kujaa maji na ndipo katika kujitetea tumeokoka watu wanne lakini mtoto wetu mmoja aitwae Sefu Abdala mwenye umri wa miaka minne hajapatikana,” alisema.
Majeruhi mwingine, Emmanuel Mniga mkazi wa mkoani Morogoro, ambaye amelazwa katika wodi ya A1, alisema alipanda jahazi hilo kwa lengo la kupelekwa biashara Pemba ambayo hata hivyo hakuweza kuitaja.
“Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake alilazimika kisimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha upepo na baadae tukaondoka lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa na wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadae kikajaa maji na kukatika katikati, “ alisema Mniga.
Aliongeza, “Mimi nilijiokoa kwa kushikilia kamba ngumu ambayo ilikuwa imefungia sehemu ya turubai katika chombo hicho hadi nilipookolewa...Kwa kweli namshukuru Mungu, “alisema.
Hata hivyo, mmoja wa wakazi aliyejitambulisha kama Hamadi Ali Hamadi, mkazi wa Sahare Kijijini, alimweleza mwandishi wetu kwamba yeye ni ndugu wa karibu wa nahodha wa jahazi hilo, Badru Mohamed alidai kwamba ajali ilitokea katika mwamba wa Nyuli katika Bahari ya Hindi jijini Tanga.
Alisema, “Jana usiku wa saa sita nilishuka bandarini Sahare kukagua jahazi hiyo kabla ya kuanza safari yake ambapo nilikuta ikiwa na abiria 32, gunia 20 za pumba, maharage kilo 60 ambazo zilikuwa zimefungashwa katika polo 25 pamoja na masanduku (kreti) 100 za vinywaji aina ya bia...kwenye safari hiyo ndugu zangu walikuwa jumla yao ni wanne, “ alisema.
“Nimepita kukagua miili nimebaini mwili wa nahodha kwamba ni mmoja wa marehemu lakini ndugu zangu wengine watatu wote wapo hai... Nilipozungumza nao wamenieleza kwamba marehemu Badru (nahodha wa chombo ) aliondoka akiwa na mabaharia (wasaidizi) wake wanne ambao binafsi siwafahamu kwa majina ambapo inasemekana dhoruba ndiyo ilipiga chombo na kukatika katikati, “ alisema.
Hata hivyo, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchikavu na Majini mkoa wa Tanga, alisema atatoa taarifa rasmi leo kwa vyombo vya habari kuhusu ajali hiyo.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela kwa vifo vya watu 12 vilivyosababishwa na kuzama kwa jahazi waliyokuwa wakisafiria kutoka Tanga kwenda Pemba.
Katika salamu zake, Rais alisema ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika kisiwa cha Jambe kilichopo katika Bahari ya Hindi umbali mfupi kutoka Tanga mjini, ambapo pamoja na vifo vya watu hao watu wengine 33 wamenusurika na 25 kati yao wamelazwa katika Hospitali ya Bombo Mkoani Tanga.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii ya kuzama jahazi, tumepoteza wapendwa wetu, watoto wetu na watu wazima ambao kwa hakika familia zao ziliwategemea katika maisha ya kila siku, nakuomba Mkuu wa Mkoa unifikishie pole nyingi kwa familia za marehemu wote na jamaa zao,” alisema Rais Magufuli katika salamu hizo za pole, zilizotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, Rais amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na pia amewataka wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki cha huzuni ya kuondokewa na jamaa zao.
Magufuli pia amewatakia matibabu mema majeruhi wote, walionusurika katika ajali hiyo ili wapone haraka, warejee katika familia zao na waendelee na ujenzi wa Taifa.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE-habarileo TANGA
Social Plugin