AMA kweli ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.... Katika hali isiyotarajiwa chui wa ajabu amezua taharuki kubwa kwa wagonjwa na wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa baada ya mnyama huyo kuibuka katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumzia juu ya tukio hilo muunguzi mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa Rustica Tung’ombe alisema tukio hilo limetokea majira ya saa 7 na saa 8 usiku wa kuamkia leo Jumatano na kwamba chui huyu alionekana nje eneo la wodi namba 6 .
Alisema kw mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na muuguzi msimamizi wa zamu usiku ni kwamba wanawake ambao walikuwa wakitoka kunyonyesha watoto wao wodini walikimbia huku wakipiga kelele za kuomba msaada baada ya kukutana na chui huyo.
"Kulikuwa na kundi la kwanza la akina mama waliotoka kunyonyesha watoto wao lilipita eneo hilo na kundi la pili lilifuata na mwanamke mmoja kati yao alikuwa nyuma akifuata wenzake na ndipo alipomshuhudia chui huyo na kuanza kupiga kelele ……wauguzi walipochungulia madirishani walipata uhakika kuwa mnyama huyo ni chui ", alisema.
Kutokana na kuwa na uhakika juu ya mnyama huyo kuwa ni chui walilazimika kuomba msaada kwa askari magereza ambao wamepakana na hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa msaada.
Alisema baada ya kufika askari magereza pamoja na kundi kubwa la wananchi kwa ajili ya kupambana na chui huyo ghafla mbwa aliibuka nyuma ya chui huyo na kuanza kumfukuza chui huyo ambaye aliruka ukuta wa uzio na kutoweka kusikojulikana.
“Wakati askari magereza wanajiandaa kupambana na chui huyo alitokea mbwa ambaye kweli hatujui alitokea wapi na kuanza kumfuatilia chui huyo ….. hili ni tukio la aina yake na halijapata kutokea katika Hospitali hii maana hapa ni mjini na hatujui chui huyu kafikaje hapa”
Na MatukiodaimaBlog
Social Plugin