Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo ameiomba Serikali kufanya tathmini ya haraka kubaini upungufu wa chakula nchini uliosababishwa na ukame wa muda mrefu.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumweka wakfu Askofu wa Dayosisi ya Meru, Elias Nassari katika Usharika wa Usa River, Wilaya ya Arumeru alisema kuwa Serikali haitakiwi kungoja hadi watu wafe ndiyo waanze kutafuta chakula.
Dk Shoo ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa kuwaandikia maaskofu wote wa kanisa hilo kuwataka waumini wao wafanye maombi, hija, mfungo kwa lengo la kukabiliana na ukame unaolikabili taifa.
Vilevile, hivi karibuni Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) lilitoa wito kama huo kwa waumini wake, huku Serikali ikisisitiza kuwa hakuna njaa nchini na kuwa haitatoa chakula cha msaada.
Askofu Shoo aliitaka Serikali iwajibike kufanya tathimini za haraka ili kubaini watu walioathirika na njaa pamoja na kujua idadi kamili ya familia pamoja na kaya zitakazoathirika na njaa ili kupata kiwango sahihi cha misaada ya chakula kitakachoitajika nchini.
“Mikoa ya Kaskazini njaa ni tishio, kuna familia tunajua hazina chakula na tumeanza kutoa misaada,” alisema Dk Shoo.
Hata hivyo, alisema kama kanisa wataendelea kufanya maombi ya mvua lakini ameitaka Serikali kuchukulia suala la ukame kwa umakini kwa kuwa viashiria vya kuwepo na njaa nchini vimeanza kuonekana.
Awali, akizungumza kwenye ibada hiyo, Dk Shoo aliwataka viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kutokuwa na kiburi pindi wanapopata madaraka badala yake wawatumikie waumini na wananchi kama walivyopewa dhamana hiyo.
“Kiburi ni tishio sana hasa pale kiongozi atakapoonyesha, tuombe Mungu sana tabia hiyo isiwepo kwa viongozi wetu wa makanisa na taasisi mbalimbali nchini,” alisema Dk Shoo katika ibada iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Viongozi waliokuwapo ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro na wabunge Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki.
Alipopata fursa ya kuzungumza, Gambo ambaye alimwakilisha Rais John Magufuli aliyataka makanisa yote nchini kuwashauri wananchi wake kuweka akiba ya chakula ili kukabiliana na ukame uliopo kwa sasa.
Pia aliwataka wawashauri wananchi kupanda mazao ambayo yanastahimili ukame ili kuepusha tishio la njaa linalotokana na ukame na wakulima ambao wanasafirisha mazao nje ya nchi kuacha mara moja.
Kuhusu migogoro ya ardhi inayoendelea nchini, Gambo alizitaka taasisi za kidini kuyalinda maeneo yao akisema kumezuka mtindo kwa baadhi ya watu kuingilia maeneo ya taasisi hizo.
Akitoa shukrani baada ya kusimikwa, Askofu Nassari aliwataka viongozi mbalimbali wa kidini kuhakikisha malengo ya kanisa yanatimia.
Pia alisema atashirikiana na viongozi wa kisiasa na kijamii kuhakikisha changamoto mbalimbali za kijamii zinatatulika.
Chadema kugawa chakula
Wakati huohuo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa alisema kwa kuwa Serikali haina utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa tatizo la chakula nchini, chama chake kitaandaa utaratibu wa kuhakikisha chakula kinapatikana.
Alisema Chadema ina uwezo wa kuomba chakula hata kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha hakuna mwananchi atakayepoteza maisha kwa tatizo hilo.
Alisema hayo katika hotuba yake aliyoitoa mjini Bukoba kwa viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya matawi hadi wilaya.
Alisema jambo kubwa linalomvutia kwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump ni uwezekano wa kuwabana viongozi wa Afrika wanaochezea demokrasia.
“Nawaambia viongozi wa dunia wajue demokrasia ni lazima ipewe nafasi yake katika nchi za Kiafrika na si kuacha iendelee kuchezewa,”alisema Lowassa aliyegombea urais akaibuka wa pili nyuma ya Rais Magufuli mwaka jana.
Pia, Lowassa aliwaeleza kuwa haina maana kusema kuna amani na utulivu wakati hakuna demokrasia na kudai kinachoendelea nchini kwa sasa ni kuwajenga hofu wananchi.
“Kinachofanyika hivi sasa ni kujenga watu hofu na kupandikiza chuki, kufanya hivyo ni kujenga mazingira ya udikteta,” alifafanua Lowassa.
Pia, alikosoa matamko yanayotolewa na Rais Magufuli akisema haoni kama yanazingatia ushauri wa wataalamu wengine.
Alidai kuwa hakuna sababu ya kujivunia ununuzi wa ndege mpya wakati kuna matatizo mengine sugu yanayowatesa Watanzania.
“Rais anatakiwa kutumia wataalamu kabla ya kutoa misimamo yake sioni sehemu anaposhauriwa na mawaziri, sioni cabinet inayomshauri kuhusu suala la njaa,” alisema Lowassa aliyewahi kuwa waziri mkuu.
Alisema ununuzi wa ndege ungesubiri na badala yake fedha hizo kutatua tatizo la maji linalowakabili wananchi wengi huku akirejea alivyoshughulikia tatizo hilo akiwa Waziri wa Maji.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Profesa Mwesiga Baregu alisema nguvu kubwa inayotumika kubana vyama vya upinzani inatia shaka na kujenga hofu kwa wananchi.
Alitoa mfano wa nguvu kubwa iliyotumika kuzuia mikutano ya Ukuta kuwa ni dalili za kutojiamini kwa Serikali kiasi cha kuvuruga utaratibu wa kidemokrasia.