Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amewasimamisha kazi watendaji watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, ili kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha zaidi ya sh. milioni 300, zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya maendeleo wilayani humo.
Waliosimamishwa kazi ni pamoja na mweka hazina, mchumi na Mhandisi wa Halmashauri hiyo. Kwa pamoja wanadaiwa kubadili matumizi ya fedha za kutekeleza miradi ya SEDEP, zilizotolewa na benki hiyo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi wa shule za sekondari.
Akizungumza akiwa katika ziara wilayani humo juzi, Mongela alisema ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike, kwani thamani ya vyumba vya madarasa na vyoo vilivyojengwa kutokana na fedha za mradi huo, hailingani na fedha zilizotumika.
“Kunzia Jumatatu (leo), kuna timu ya wakaguzi itakuja hapa Magu kukagua na kuchunguza thamani ya fedha zilizotumika kwenye miradi hii ambayo nimeikagua. Miradi hii inajumuisha miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo ambayo inaonyesha wazi kuna uchakachuaji umefanyika,”alisema Mongela.
Mkuu Wilaya ya Magu, Hadija Nyembo alisema mambo yaliyokwamisha miradi ya ujenzi huo ni kuelekeza fedha hizo katika ujenzi wa maabara tofauti na matumizi ya fedha yalivyopangwa.
Hata hivyo, mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo, yanadaiwa kuwa yalifanyika bila kuthibitishwa na Wizara ya Fedha na Mipango ili yapewe baraka kwa kuwa Wizara hiyo, ndio yenye mamlaka ya kutoa idhini ya mwisho ya matumizi ya fedha za Umma.
Kutokana na sababu hizo mkuu huyo wa Mkoa aligoma kuzindua vyumba viwili vya madarasa vya shule ya msingi Nyanguge vilivyojengwa kupitia kiasi hicho cha fedha, kutokana na madai kuwa vyumba hivyo pamoja na ujenzi wa vyoo vimejengwa chini ya kiwango.