Mtoto mwenye umri wa siku moja mwenye jinsia ya kiume amefariki dunia baada ya kutupwa na mtu asiyefahamika katika tundu la choo la Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) lililopo Kitangiri manispaa ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Januari 20,2017 saa 11 jioni ambapo waumini wa kanisa hilo walisikia sauti ya mtoto ikitokea katika tundu la choo cha kanisa.
Akisimulia kuhusu tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa Kitangiri Habiba Jumanne alisema alipigiwa simu na baadhi ya waumini wa kanisa hilo kuwa kuna sauti ya mtoto mchanga inasikika kutoka ndani ya tundu la choo.
“Tulifanya jitihada za kuvunja choo na kumtoa mtoto akiwa hai tukamkimbiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga cha kusikitisha leo asubuhi Januari 21,2017 tumekwenda kuona hali ya mtoto,daktari ametueleza kuwa mtoto amefariki dunia”,alisema Jumanne.
Jumanne alisema baada ya kuvunja choo hicho na kumtoa mwili wake ulikuwa umetapakaa kinyesi hivyo walimuogesha maji ya baridi huenda maji hayo yamechangia kupatwa na baridi kali na kusababisha kupoteza uhai wake.
Mwenyekiti huyo alisema mpaka sasa mtu aliyefanya kitendo hicho hajajulikana na wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kama kuna mkazi wa eneo hilo ndiyo kahusika na kwamba tayari wameomba kibali kutoka cha polisi ili kwenda kuzika mwili wa mtoto huyo kwa kushirikiana na kanisa la AICT.
Hata hivyo alitoa wito kwa jamii kuacha mara moja vitendo vya kinyama na kama wanaona maisha magumu kulea watoto wawapeleke kwenye mashirika au taasisi za kulea watoto wakapate kukua kuliko kutenda unyama wa mauaji
Hata hivyo Mzee wa kanisa la AICT David Madata alisema wakati akifundisha watoto somo la Injili kanisani hapo alimuona mwanamke mmoja aliyekuwa amelala karibu na choo hicho lakini hawakumdhania kama atafanya unyama huo baada ya muda aliondoka kusikojulikana na kuanza kusikia sauti ya mtoto mchanga kwa waliokuwa wakienda chooni hivyo waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi na serikali ya mtaa.
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga SSP Elias Mwita alisema mtoto huyo alitupwa kwenye tundu la choo la kanisa la AICT na mtu ambaye hajafahamika na wanaendelea na uchunguzi kumbaini aliyehusika na kitendo hicho.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin