MUUGUZI WA HOSPITALI YA WILAYA AFARIKI AKICHOTA MAJI TARIME

MUUGUZI wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Magreth Anatoly (57), amefariki dunia kwa shinikizo la damu wakati alipokuwa akisomba maji kutoka kwenye tangi la lori lililokuwa limepeleka maji katika hospitali hiyo, ambayo imekumbwa na ukosefu mkubwa wa maji.

Mfanyabiashara na kada wa CCM, Peter Zakaria amejitolea kutoa lori lake lenye tangi la maji kupeleka maji katika hospitali hiyo pamoja na Magereza wilayani hapa.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ya wilaya, Calvin Mwasha amethibitisha kufariki kwa muuguzi Magreth, na kueleza kuwa alifariki Alhamisi mchana wakati muuguzi huyo akiwa na wenzake, walipokuwa wakisaidia kazi ya kusomba maji kwa kutumia ndoo kutoka kwenye tangi la lori, lililokuwa limepeleka maji ya matumizi hospitalini hapo.

“Muuguzi huyo alipofikisha ndoo aliyokuwa amebeba alikaa kwenye kiti kupumzika na kujisikia hali yake kuwa mbaya na kudondoka chini na kusaidiwa na wenzake waliokuwa naye, lakini alipoteza maisha. Kifo chake kimetokana na shinikizo la damu. Tumepata pigo kubwa kwa mama yetu Anatoly kwani alikuwa kiungo kikubwa kwetu hususani vijana wanaoanza kazi,” alieleza daktari wa wilaya.

Muuguzi huyo alizikwa mjini Tarime jana.

IMEANDIKWA NA SAMSON CHACHA,-habarileo TARIME

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post