MKUU wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga amesema amepiga marufuku ya kuweka kioo cha giza sehemu ya mbele ya gari kwa sababu trafiki wanapata shida kuwaona madereva wanaoendesha magari hayo na pia huwa katika hatari ya kusababisha ajali barabarani.
Mpinga pia amesema kwamba agizo lake kuhusu kuwataka walioweka taa zenye mwanga mkali kwenye magari yao, linahusu taa zote zikiwemo zilizowekwa na wamiliki kama urembo pamoja na zile zilizowekwa kwenye magari hayo viwandani zilizokotengenezwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mpinga alitoa mfano wa dereva mmoja aliyemgonga askari wa kike wa usalama barabarani aliyekuwa anaongoza msafara kutokana na dereva huyo kuweka kioo cha giza cha mbele na hivyo kutoweza kuona kikamilifu.
“Kama utakumbuka miaka michache iliyopita askari wetu wa kike aligongwa pale Bamaga, tulifuatilia na kubaini kuwa dereva aliyemgonga kuna uwezekano hakuwa anaona vizuri kutokana na kuweka kioo tinted (cha giza) cha mbele,” alisema Mpinga.
Askari huyo aliyejulikana kwa jina la Elikiza alikuwa akiongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete na baada ya msafara huo, aliruhusu magari mengine yaendelee na safari, ndipo ghafla gari aina ya Landcruiser VX lilipotoka upande wa pili na kumgonga wakati trafiki huyo anasimamisha magari.
Alisema hata hivyo polisi haina takwimu za ajali ambazo zimesababishwa na kuwepo kwa magari yenye vioo vya giza,
“Takwimu hapa sina maana tumekuwa tunachukua tu takwimu kwa madereva walevi, mwendo kasi na sababu zingine, lakini hiyo ya tinted kwa sasa hatuna ila ninachosema ni hatari kwa usalama wa barabarani.”
Mpinga alisema pamoja na tukio hilo, askari wa usalama barabarani wamekuwa wakipata usumbufu wanaposimamisha magari yenye vioo vya giza mbele kwa kuwa hawamwoni anayeendesha gari.
“Wakati mwingine magari hayo yenye tinted kioo cha mbele wanaendesha watoto ambao hawaruhusiwi kuendesha magari, na akisimamishwa dereva huyo mtoto anaweza kubadilishana na mtu mwingine aliyembeba,” alisema Mpinga.
Aliongeza kuwa askari anamwona anayeendesha gari pale tu dereva anapofungua dirisha. Alisema kwa sheria za usalama barabarani dereva anatakiwa aonekane hata kama amefunga vioo vya pembeni.
Alisema hata wale ambao wameweka vioo vya giza mbele wanapata wakati mgumu kuona na ndio maana wakati mwingine wanalazimika kutoboa ili aone kupitia vioo vya pembeni.
“Hii kwa usalama barabarani pia hairuhusiwi, unaweka tinted kali kiasi hicho unaficha nini?’’ Alihoji Mpinga. Kuhusu magari yaliyowekwa taa kali, Mpinga alisema baada ya kutoa agizo la kuwataka wamiliki kuondoa taa hizo kwenye magari yao alipokea maoni ya kuomba taa zilizowekwa kiwandani ziachwe kwa sababu hazikuwekwa na wamiliki.
“Lakini sisi tumeona kwamba taa hizo zenye mwanga mkali ambazo zimewekwa kiurembo ziondolewe zote, hata zile ambazo zimewekwa huko kiwandani,” alisema Mpinga na kufafanua kuwa atatoa taarifa zaidi leo atakapozungumza na waandishi wa habari. James Yohana ni mmoja wa madereva ambao wameweka vioo vya giza mbele ya gari lake alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo alisema, “Mimi niliweka kwa sababu tu sipendi kuonekana kwa watu ninapoendesha gari, sina sababu nyingine,” alisema.
Alipoulizwa kama anafahamu kwamba gari zenye vioo giza zimepigwa marufuku na polisi alisema kwamba anafahamu na tayari moja ya gari lake ameshaondoa kioo cha giza na kwamba sasa atafanya hivyo katika gari lake la pili.
Naye Abdul Muyanga mkazi wa Kipunguni Dar es Salaam alipoulizwa sababu ya kuweka kioo cha giza sehemu ya mbele ya gari lake alijitetea kwamba alifanya hivyo ili kujikinga na jua pamoja na kupendezesha gari lake.
“Mimi nilifanya sio kwa nia mbaya, niliweka kujikinga na jua, lakini pia ukiweka tinted mbele na kwenye vioo vya milangoni gari inapendeza,” alisema Muyanga.
Aliongeza kuwa baada ya tangazo la kamanda Mpinga, anachofanya siku hizi akifika kwenye taa za usalama barabarani anafungua madirisha yote ili trafiki waweze kumwona anayeendesha gari.
Hivi karibuni Mpinga alitangaza kuzikamata gari zote ambazo zimeweka vioo vya giza mbele. Pia aliagiza magari yote ambayo yamewekwa taa za zenye mwanga mkali kuziondoa mara moja kwa kuwa zinawaumiza madereva wengine na kusababisha ajali.
Chanzo-Habarileo
Chanzo-Habarileo
Social Plugin