Rais wa Jmamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Shinyanga kumfutia usajili mwekezaji wa Kiwanda cha Nyama, Kampuni ya Triple S na badala yake watafute mwekezaji mwingine.
Agizo hilo limetolewa leo Mjini Shinyanga wakati akiwahutubia wananchi wa mji wa huo ambapo yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi iliyoambatana na sherehe ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
“Futeni usajili wa mradi wa Triple S, haiwezekani mwekezaji akashindwa kuendesha kiwanda kwa zaidi ya miaka 10 sasa afu tuendelee kumkumbatia, tafuteni mwekezaji mwingine, mkishindwa semeni Serikali iweke hela, ili uzalishaji uendelee,” alisisitiza Rais Magufuli.
Aliongeza kuwa mwekezaji huyo amekuwa mbabaishaji kwani tangu kipindi yeye (Rais Magufuli) alipokuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo alimfahamu na alimpa maelekezo cha kusikitisha hakuna jambo aliloendeleza ikiwemo kuanza kwa uzalishaji.
Akizungumzia sababu ya kufanya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar katika upande huu wa Bara Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni moja, na kuongeza kuwa chimbuko halisi la uwepo wa Taifa la Tanzania ni Mapinduzi ya Zanzibara mabapo miezi michache tu baada ya kufanyika kwa mapinduzi hayo Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzaliwa kwa Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI na Kazi maalumu kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Haji Omari Heri amesema wao kama Wazanzibar wamefarijika sana kwa kitendo cha Serikali ya Awamu ya Tano kuamua kushiriki maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu kwa kusherehekea katika upande wa Bara kitu ambacho akijawahi kufanyika kabla.
Aliongeza kuwa ujio wake umetokana na ukweli kwamba Tanzania ni nchi moja hivyo Rais Magufuli alivyoeleza nia yake ya kuadhimisha Mapinduzi huku Bara, Rais Dkt. Shein alimteua aje kumwakilisha na kueleza kuwa maefarijika sana na kusema Tanzania ni yetu sote na tutaendelea kuwa wamoja.
Rais Dkt. Magufuli yuko ziarani Mkoani Shinyanga ambapo kesho anatarajiwa kufungua viwanda kadhaa vilivyopo mkoani hapo, baadhi ya viwanda hivyo ni pamoja na Kiwanda cha Vinywaji Baridi (maji) cha Jambo, Kiwanda cha Mafuta na vingene.
Na: Frank Shija - MAELEZO.
Social Plugin