Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, tarehe 28 Januari, 2017 ameondoka nchini na kuelekea Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ambako atahudhuria mkutano kilele wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea nchini humo.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli ameagwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa na Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Bw. Paul Makonda.
Pamoja na kuhudhuria Mkutano huo, akiwa Addis Ababa Rais Magufuli anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Bara la Afrika wanaohudhuria Mkutano huo.
Hii ni ziara ya kwanza ya Mhe. Rais Magufuli nje ya Afrika Mashariki tangu aingie madaraka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 05 Novemba, 2015
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Januari, 2017
Social Plugin