WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Ametia agizo hilo leo (Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.
Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“Katika halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya leo atakuwa amejifukuzisha kazi.
Aidha, ameagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Pia amewataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Social Plugin