Muujiza !! WACHIMBAJI 15 WALIOFUKIWA NA KIFUSI MGODINI GEITA WAOKOLEWA... WASIMULIA WALIVYONUSURIKA KUFA...INATISHA SANA


Mmoja kati ya wachimbaji wa madini 15 waliokuw wamefukiwa na kifusi kwenye mgodi wa RZ Union mkoani Geita baada ya kutoka shimoni akipokelewa na askari wa jeshi la zima moto na uokoaji na wananchi-Picha zote kwa Hisani ya Madukaonline blog

Raia wa kichina akipanda sehemu ya juu baada ya kuokolewa kwenye mgodi wa RZ Union mkoani Geita
Wananchi wakishangilia kwa Furaha baada ya zoezi la uokoaji kuwa limefanikiwa
Wananchi wakifuatilia shughuli ya uokoaji.
Majeruhi wakipatiwa Huduma ya kwanza.
Mkuu wa mkoa wa Geita Meja jenerali Mstaafu,Ezekiel Kyunga akiwashukuru wananchi kwa utulivu waliouonesha.
Naibu Waziri wa nishati na madini akizungumza na wananchi wa Nyarugusu na kuwashukuru
Moja kati ya wafadhili waliojitolea kutoa huduma kwenye ajali hiyo na mkurugenzi wa Waja,Chacha Mwita akielezea namna ambavyo wameshiriki kutoa huduma

Mbunge wa CHADEMA ,Upendo Peneza akielezea namna serikali inavyotakiwa kuwajibika kuwa na vifaa vya uokoaji
Raia wa China baada ya kuokolewa




Zoezi la uokoaji kwa wachimbaji kumi na tano (15)Kwenye mgodi wa RZ Union uliopo kijiji cha Mawemeru kata ya Nyarugusu limekamilika huku watu wote waliokuwa wamefukiwa wakitoka wakiwa salama baada ya kuishi ardhini kwa muda wa takribani siku nne.

Zoezi la uokoaji lilianza tangu Januari 26,2017 majira ya saa nane usiku baada ya ofisi ya madini Mkoa kupatiwa taarifa na kuweza kufika katika eneo la mgodi ambao unamilikiwa na wachina lakini leseni ikiwa inaonesha umiliki kwa mchimbaji mzawa ambaye ni Bw, Ahmed Mbaraka.

Tarehe 28.01.2017 majira ya saa moja jioni wakati wakiendelea na shughuli baadhi ya waokoaji walisikia sauti ya wachimbaji hao wakigonga bomba ambalo lililokuwa likitumika kupitisha hewa na baada ya kujua wapo maeneo hayo kilichofanyika ilikuwa ni kuwapelekea Radio Koo ,ambayo ingeweza kusaidia mawasiliano.

 Hata hivyo juhudi hizo hazikuweza kuzaa matunda kutokana na kushindwa kupatikana kwa mawasiliano.

Kufuatia ya hatua hiyo kushindikana ilibidi waandikiwe ujumbe wa maandishi ambao ulitumwa kwa njia ya bomba wakiulizwa wanaendeleaje pamoja na kalamu ya kujibu ujumbe huo.

Wachimbaji hao wakiwa chini ya ardhi walisema wapo salama na wapo kumi na tano kubwa zaidi wanaomba kupatiwa soda,sigara,biskuti pamoja na uji lakini mwenzao mmoja alichomwa na msumari.


Shughuli ya uokoaji imemalizika siku ya leo Januari 29,2017 majira ya saa tatno ambapo baada ya kuokolewa walipatiwa huduma ya kwanza kwenye maeneo hayo ya mgodi na kisha kupelekwa Hospitali ya mkoa wa Geita  kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

BAADHI YA MAJERUHI WAMEZUNGUMZIA NAMNA AMBAVYO WALIKUWA WANAISHI CHINI YA ARDHI.

Dickson Moris, ambaye ni mkazi wa Nzega mkoani Tabora ameeleza kuwa waliingia kwenye shimo hilo juzi muda wa saa nane usiku na wakati wakiendelea na shughuli walisikia umeme umekata hali ambayo walijua kuwa wamekwisha kufukiwa hadi wanapata mawasiliano hali yao ilikuwa ni mbaya zaidi.

Naye Augustino Robert ameeleza kuwa yeye alikuwa chini mbili wakati anatoka kuja chini moja kwa ajili ya kutoka ndipo walipokuta shimo limejifukia.

Amesema  hali hiyo iliwafanya wakate tamaa na kujua kuwa ndiyo mwisho wa maisha yao lakini hata hivyo bado waliendelea na jitihada za kutaka kujiokoa na baada ya kujaribu kuchimba walikutana na gril ambayo ilikuwa inaleta bomba kwa chini na ndipo walipoligonga na kuomba msaada.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI DR,MEDARD KALEMANI.

Akizungumza na wananchi baada ya kukamilika kwa zoezi zima la uokoaji, Naibu waziri wa nishati na madini,Mh Medard Kalemani ameshukuru kwa wachimbaji wote kutoka salama na amemtaka kamishina wa madini kanda ya ziwa kufanya tathmini ndani ya muda wa siku tano na shughuli ziwe zimesimama na baada ya kukamilika ndiyo shughuli za uchimbaji zitaendelea.


“Lazima maeneo tunayofanyia kazi yawe salama kwa wananchi wetu ili watu wasipoteze maisha yao, eneo ambalo limetokea ajali tumelifukua fukua hivyo sio salama sana kutokana na hili nitamuacha Kamishina wa madini afanye shughuli ya tathmini siku tano”,alisema Kalemani.


Katika hatua nyingine Kalemani amemwagiza kamishina wa madini kumchukulia hatua mkaguzi ambaye alitakiwa kukagua na hakukagua mgodi huo.

“Na mkaguzi ambaye alitakiwa kukagua na hakukagua namwagiza kamishina wa madini kumchukulia hatua za kisheria na hatua ya pili tutapita kutambua maeneo ambayo yanamilikiwa na hayafanyiwi kazi ,kupatiwa wachimbaji wadogo ili waendelea na shughuli za uchimbaji”,alisisitiza Kalemani.

MBUNGE WA VITI MAALUM UPENDO PENEZA AOMBA SERIKALI

Mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Upendo Peneza,ameiomba serikali kuwa na utaratibu wa kuwa na vifaa vyao na kuachana na dhana ya kutegemea vifaa kutoka kwa wachimbaji wengine pindi ambapo tatizo linatokea na kuacha kutegemea kutoka kwenye mashirika mengine.


“Naomba serikali iwe na desturi ya kuwa na vifaa vyake na kuacha kutegemea mashirika binafsi maana hawa watu kama GGM na BUSWOLWA MEN,wamejitolea vifaa nadhani ni vizuri serikali ikawa na vifaa vyake na timu ambayo itasaidia kuokoa,  hawa watu wamefanya kwa upendo tu kwani haikuwa ni lazima”,alisema Peneza.

MKUU WA MKOA WA GEITA
Mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu,Ezekiel Kyunga amewashukuru wananchi kwa utulivu waliouonesha pamoja na makampuni yote yaliyoshiriki kufanikisha zoezi la uokoaji.


MAKAMPUNI AMBAYO YAMEFANYA ZOEZI ZIMA LA UOKOAJI

Makampuni hayo kampuni ya Buswolo Min,GGM pamoja na baadhi ya wachimbaji wadogo waliopo kwenye eneo hilo wakishirikiana na jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Geita.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post