VILIO, majonzi na simanzi vilitanda katika baadhi ya mitaa ya jijini Tanga ikiwemo Chumbageni na Nguvumali wakati msafara wa pikipiki na magari uliochukua mwili wa marehemu Salim Kassimu (18) mkazi wa Mwamboni jijini Tanga anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mwili wa Salim ulikuwa ukitolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo ili kupelekwa nyumbani kwao eneo la Transfoma Mwamboni na baadaye kuhifadhiwa kwenye makazi yake ya milele baada ya kukabidhiwa kwa familia yake na kuzikwa jana asubuhi katika makaburi yaliyoko Masiwani Shamba.
Mjomba wa Marehemu, Abdi Shabani alisema walikabidhiwa mwili huo mara baada ya uc hunguzi wa Polisi kukamilika.
Baadhi ya wakazi walipozungumza katika mahojiano na mwandishi walisema marehemu huyo alikuwa akifanya kazi ya ukondakta wa daladala inayosafiri kati ya Nguvumali na Raskazone jijini hapa na inadaiwa alifia njiani wakati alipokuwa akipelekwa hospitali kupata matibabu baada kutekwa kwa saa kadhaa na kisha kupatiwa kipigo na baadaye kutekelezwa nje ya nyumba yao Mwamboni.
Huduma za daladala kutoka Kituo cha Nguvumali kuelekea maeneo ya katikati ya mji zililazimika kusitishwa kuanzia asubuhi kwa kile kinachodaiwa na madereva na makondakta kwamba ni kuomboleza msiba wa mwenzao huyo ambaye wanadai ameuawa kikatili.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuchukua mwili huo, Meya wa Jiji la Tanga, Mhina Mustafa Selebos aliwasihi wakazi hususan wa Kata ya Nguvumali kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.
“Naomba wananchi tuwe wavumilivu wakati huu ambapo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kifo cha huyu ndugu yetu... Kipekee nimpongeze sana Kamanda wa Polisi kwa ushirikiano alioutoa hadi kuwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa, nawaomba tuvute subira ili sheria iweze kufuatia, “alisema.
Naye mama mlezi wa marehemu, Salma Mnyamisi akizungumza mara baada ya mwili kufikishwa nyumbani alisema mwanaye amekufa kifo cha kinyama.
“Kwa kweli kifo cha mwanangu huyu ni cha kinyama naiomba serikali iingilie kati ili wahusika wa tukio la mauaji haya waweze kupatikana na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Mwombolezaji Bwanaheri Athumani alisema amesikitishwa na tukio hilo la watu hao kujichukulia sheria mkononi na kuiomba serikali kuingilia kati ili kukomesha vitendo hivyo.
Naye Habibu Tunda alisema kumekuwepo na mwendelezo wa matukio ya uhasama na visasi baina ya raia na baadhi ya askari wa JWTZ wanaoishi katika kambi iliyopo Kata ya Nguvumali ambavyo mara kadhaa vimesababisha watu kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara kwa wakazi wa maeneo yanayozunguka kambi hiyo.
“Ili kukomesha ukatili huu tunaofanyiwa na hawa jirani zetu tunaomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wahusika wote bila kujali nyadhifa zao, “alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amethibitisha tukio hilo na kwamba watu watatu (majina yamehifadhiwa) wanashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE-habarileo TANGA
Social Plugin