WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji awakamate maofisa wanne wa Chama Kikuu Cha Ushirika (MAMCU) na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi wa Polisi kujibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.
Kufuatia agizo hilo, Polisi imewatia mbaroni watuhumiwa hao na juzi walipandishwa katika karandinga la jeshi hilo na kupelekwa Masasi. Maofisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Lawrence Njozi.
Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Yusuph Namkukula na Ramadhani Namakweto.
Majaliwa alifikia uamuzi huo juzi jioni kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO-Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.
Katika kikao hicho, Majaliwa alitaka maelezo ya kina ni wapi zilipo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompa viongozi hao ilionesha waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.
Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani.
“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha ikionesha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.
Tuhuma zinazowakabili maofisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo.
Mfano wa suala hilo ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali. Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa Novemba 10, 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.
Tuhuma nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwaka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.
Dai jingine linalowahusu maofisa hao ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).
Kutokana na mapungufu hayo, Majaliwa aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike.
Waziri Mkuu pia alimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.
Awali, wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima walisema wana kero nyingi kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati, kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.
“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa.
Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.
Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3,mwaka huu katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Rais John Magufuli.
Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye (Waziri Mkuu) hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.
Chanzo-Habarileo
Chanzo-Habarileo