NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameonya kuwa watu wakiwemo wanasiasa wanaoeneza taarifa za uongo za kuwepo kwa baa la njaa, ni kosa na wachukuliwe hatua ikiwemo kukamatwa.
Masauni amesema bado kuna watu wanajichukulia mamlaka ambayo sio yao na kueneza uongo kuwa kuna njaa nchini, hilo ni kosa kwa kuwa kwa kueneza propaganda hiyo kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
“Hizo ni propaganda za watu wasioitakia mema nchi hii ….. mtu anapofanya kosa lazima achukuliwe hatua …… Jeshi la Polisi liangalieni hili,” alisisitiza.
Masauni alitoa onyo hilo wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya jana mkoani Rukwa ambako Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven alimhakikishia kuwa mkoa huo hauna njaa, bali una ziada ya kutosha.
“Nyie wenyewe mmemsikia mkuu wa mkoa (Zelothe) amethibitisha kuwa hakuna njaa mkoani hapa lakini sio hapa tu, pia mikoa ya Mbeya na Songwe wamenithibitishia kuwa hawana njaa,” alisema Naibu Waziri Masauni na kuongeza: “Sasa wapo wanasiasa uchwara wanaeneza propaganda kuna njaa, sio mamlaka yao kutangaza kuwa kuna njaa, kueneza uongo kama huo ni si sawa kwa kuwa kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini, wanastahili kuchukuliwa hatua ikiwemo kukamatwa,” alisisitiza.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe alimweleza Naibu Waziri Masauni kuwa hali ya kiusalama katika mkoa huo ni shwari ambapo amani na utulivu umeshamiri kwa kuwa una chakula cha kutosha.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin