Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFISA MTENDAJI WA KATA ANUSURIKA KUTAFUNWA NA FISI



OFISA Mtendaji wa Kata ya Mgongo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, Mwajuma Rugambwa (42), amejeruhiwa na fisi aliyemvamia, ambaye alipambana naye ili kunusuru uhai wake.

Tukio hilo lilitokea juzi baada ya mtendaji huyo akiwa kazini kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgongo, Humphrey Mkumbo kuhusu uwepo wa fisi huyo ambaye alijeruhi wananchi wawili ambao hadi sasa wanaendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya.

Akisimulia tukio hilo wakati akizungumza na MTANZANIA, Mwajuma alisema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa tukio hilo, alipiga kipyenga cha kuashiria hali ya hatari na wananchi walikusanyika ili kuweza kumsaka fisi huyo.

Alisema wakati akiendelea na kazi hiyo, kumbe fisi alikuwa amejificha juu ya mbuyu na ghafla alishuka na kuanza kumrarua mwilini, lakini alipambana naye na kufanikiwa kumdhibiti.

“Nilipopata taarifa hiyo nilichukua hatua ya kupiga kipyenga ili kuashiria kuna tukio la hatari. Wananchi walikusanyika kwa ajili ya kumsaka fisi huyo ambaye alikuwa amejificha kwenye pango la mti wa mbuyu.

“Kwa kuwa tulikuwa tumetawanyika kidogo, nilimuona fisi ametoka mbio na akaanza kumrarua kijana mmoja ambaye sikufahamu jina lake haraka, na mimi nikiwa na jiwe na mkoba wangu, aliponiona akaanza kunirarua na akaniangusha chini.

“Baada ya kuniangusha akaniuma paja la kulia, ghafla ujasiri ulinijia na kumkaba koo kwa mikono yote miwili, nilipomkaba akaniuma mkono wa kushoto hadi kidole kimoja kikavunjika.

“Hata hivyo sikuachilia mkono wa kulia, nilizidi kumkaba koo hadi wananchi walipokuja kunisaidia na kumuua,’’ alisema Mwajuma huku akiugulia maumivu makali.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi, Dk. Adam Mashenene, alisema juzi saa mbili asubuhi walipokea majeruhi wawili walioshambuliwa na fisi kutoka katika Kijiji cha Mgongo. 

“Majeruhi hao ni Masunga Ngusa (29) na Nkomba Ngusa (27), ambao walifikishwa hapa hospitali kwa matibabu na tuliwaingiza katika chumba cha upasuaji kuwafanyia huduma ya kwanza kwa kuwasafisha ili kuondoa uchafu katika vidonda ambavyo fisi huyo alikuwa akinyofoa kula nyama katika sehemu za miili yao na majeruhi mwingine alivunjwa mkono,” alisema Dk. Mashenene.

Alisema kwa kuwa hospitali yao haina uwezo wa kutibu majeraha hasa kufanya upasuaji mkubwa, waliwapa rufaa na kuwapeleka katika Hospitali ya Misheni ya Hydom, Mkoa wa Manyara kwa matibabu zaidi.

Dk. Mashenene alisema kutokana na tukio hilo, ilipofika saa tisa alasiri walipelekwa majeruhi wengine hospitalini hapo ambao walijeruhiwa na fisi huyo ambao ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mgongo, aliyeumwa paja la kulia na mkono wa kushoto na kusababisha kidole kuvunjika na mwingine aliyeshambuliwa mkono wa kushoto ambao hadi sasa bado wanaendelea na matibau hospitalini hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula, aliwatembelea majeruhi hao na kuwapa pole, huku akiwapongeza kutokana na ujasiri wa kupambana na fisi huyo, hasa Ofisi Mtendaji Mwajuma.

Na Seif Takaza-Mtanzania Singida

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com