Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKARI WA JWTZ WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUSABABISHA KIFO CHA KONDAKTA WA DALADALA


ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Sajini John Komba na wenzake wanne wakiwemo mgambo na wanafunzi wa jijini hapa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga kwa kosa la kusababisha kifo cha aliyekuwa kondakta wa daladala inayosafiri kati ya Nguvumali na Raskazoni, Salim Kassim (18) mkazi wa Mwamboni.

Wakili wa Serikali, Donata Kazungu akisoma shitaka hilo la mauaji linalowakabili watuhumiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Hilda Lyatuu alisema Januari 26, mwaka huu katika Kambi ya JWTZ iliyoko Kata ya Nguvumali jijini Tanga, Komba mwenye namba MT 69500 na wenzake watatu walimuua Kassim katika eneo la kambi hiyo.

Wakili Kazungu aliwataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Adam Juma (20), Sofia John (20) ambao ni mwanafunzi, Yohana Warioba na Bernard Nicholaus ambao ni wanamgambo wanaolinda katika kambi hiyo.

Hata hivyo, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji. Aidha, upelelezi kuhusu kesi hiyo haujakamilika na hivyo itatajwa tena Februari 26, mwaka huu.

IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE-habarileo TANGA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com