Katibu Mkuu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Mchungaji Jacob Mapambano akiongoza ibada maalumu ya kumsimika katika utumishi Mwinjilisti Esther Emmanuel katika kanisa la AICT Bushushu
Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Shinyanga limetangaza vita dhidi ya baadhi ya waumini wanaosababisha migogoro na chuki ndani ya kanisa na kusababisha mtafaruku na wakati mwingine baadhi ya waumini kukimbia kanisa.
Hayo yamesemwa juzi na Katibu mkuu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Mchungaji Jacob Mapambano wakati wa ibada ya kumsimika katika utumishi Mwinjilisti Esther Emmanuel katika kanisa la AICT Bushushu lililopo katika manispaa ya Shinyanga.
Alisema waumini ambao wamekuwa wakisababisha chuki na migogoro lazima washughulikiwe kwani wanakwamisha kazi ya mungu na kusababisha watumishi wa mungu wafanye kazi katika mazingira magumu.
“Kuna baadhi ya watu wanajiweka kimbele mbele,wao ni wakosoaji,wanabeza kila jambo,watafanya kila jambo ili kukwamisha kazi ya mungu,wanakwamisha mipango yetu mizuri ya kulijenga kanisa la mungu”,alieleza mchungaji Mapambano.
“Sasa tumeanza kuwashughulikia watu hawa,kama jinsi serikali inavyowashughulikia baadhi ya watu,na sisi kanisani humu tunawashughulikia tu watu hawa,maana hatuwezi kusababisha kondoo wa mungu wengine wakaondoka”,aliongeza Mchungaji Mapambano.
Katika hatua nyingine katibu huyo mkuu wa kanisa la AICT alisema katika mambo ambayo alikuwa hayaamini ni uchawi na kishirikina ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya waumini katika makanisa.
“Leo nakusimika katika utumishi Mwinjilisti Esther Emmanuel,wakati mwingine utatumika kwa watu ambao wanaamini uchawi,utatembea katika vijiji,miji ambako kuna watu wanaamini nguvu za kichawi,nakuomba usimame imara katika maombi”,aliongeza Mchungaji huyo.
“Siku nilikwenda kusuluhisha mgogoro katika moja ya makanisa yetu,wakristo wamegombana na uongozi wa kanisa,kwaya na waktisto,viongozi na kwaya,kwa mara ya kwanza nilishangaa sana kukuta kuna wakristo wakawa wameweka mtego wa kichawi kwenye njia ili nikifika nianguke,nizirai nisiweze kusuluhisha mgogoro ule”,alieleza.
“Kutokana na mtego ule wa kichawi ulitengenezwa na wakristo ndipo nilipoanza kujua kuwa kweli uchawi upo,nilipofanya kazi ile ya kusuluhisha nikaimaliza bila kujua kama kuna nguvu za giza,wakati mwingine watu wakaniogopesha lakini nilisimama imara katika mungu”,alifafanua Mchungaji huyo.
Aidha alimtaka mwinjilisti Esther Emmanuel aliyesimikwa katika utumishi kanisa la AICT Bushushu kusimama imara katika utumishi,adumu katika maombi na kuwaomba waumini wa kanisa hilo kumuombea mtumishi huyo na kumpa ushirikiano katika kufanya kazi ya mungu.
Katika hatua nyingine Mchungaji Mapambano alisema kanisa la AICT linaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais John Pombe Magufuli katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwani taifa linapoteza nguvu kazi kwa vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.
“Kuna baadhi ya watu wamejitokeza kupinga jitihada zinazofanywa na serikali kupambana na dawa za kulevya ambapo rais amekuwa akisema washindwe na walegee,mimi nasema watu hawa washindwe na wapotee kabisa kama nitakuwa nimetenda dhambi mnisamehe sana”,aliongeza mchungaji Mapambano.
Naye mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyehudhuria ibada hiyo aliwataka viongozi wa dini kufikisha neno la mungu katika maeneo ya pembezoni ili wawe na hofu ya mungu na kuacha vitendo viou ikiwemo kuua vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi.
“Serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na madhehebu ya dini,naomba muendelee kufanya kazi hii kwani mnaisaidia serikali kusaidia kuimarisha amani nan chi na tutaendelea kushirikiana nanyi”,alisema Matiro.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin