Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema haridhiki na hali aliyoikuta kwenye Kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Minjingu, baada ya kubaini kuwa wanatumia mifuko yenye nembo ya Kenya wakati mbolea hiyo inazalishwa hapa nchini.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho waandike barua kwa Rais Dk. John Magufuli kabla hajamaliza ziara yake Jumatano, awe amepata nakala ya barua hiyo.
Agizo hilo alilitoa jana baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Babati akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara. Waziri Mkuu alirejea Babati akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa na ratiba za kitaifa.
“Nilikuja kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii haikubaliki huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika inasaidia kutoa mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa kukuta mifuko ya kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati mali ghafi inatoka Tanzania.
“Ni kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone anuani ya Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya TBS. Kwa nini Tanzania haionekani? kwani malighafi iko Kenya? haiwezekani, ni lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Yeye anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi mnafanya hivyo?,” alihoji.
Akiwa ndani ya kiwanda hicho, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya mifuko ya mbolea ikiwa imeandikwa: ‘County Government of Bungoma’, ina nembo ya Serikali ya Kenya na anuani ikionesha kuwa mbolea hiyo imetengenezwa na kiwanda cha mbolea cha Minjingu lakini anuani inasomeka P. O Box 2941 – 00200 Nairobi, Kenbro Industrial Park, Mombasa Road; namba ya simu +254-20-6000-970 lakini mifuko hiyo pia ina muhuri wa TBS.
Baadhi ya mifuko ilikuwa ikipakiwa ndani ya lori tayari kwa kusafirishwa kwenda kwa wateja.
Alisema atamwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kwenda kiwandani hapo na wanasheria wake pamoja na wataalamu kutoka Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC) ili waangalie hatua gani zinapaswa kuchukuliwa.
“Kwa staili hii hii tumeona watu wakinunua kahawa yetu na kwenda kuipakia upya huku wakiweka lebo za kwao. Leo hii hata Tanzanite pia inasemwa imetengenzwa India. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee,” alisema
“Tukiruhusu hali hii, watu watajuaje kuwa mbolea hii ambayo ni first class duniani kuwa inapatikana Tanzania? Kiwanda chetu, ardhi yetu, suala la kutangaza nchi yetu kwa kutumia bidhaa zetu litafanikiwa kwa njia hii kweli?,” alisema na kuhoji
Akitoa maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Tosky Hans alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi.