Maelfu ya wakazi wa mkoa wa Mbeya wamejitokeza katika mazishi ya mchezaji wa zamani Geoffrey Bonny Mwandanji aliyefariki dunia juzi na kuzikwa katika makaburi ya kanisa Katoliki Makandana wilayani Rungwe.
Akizungumza wakati wa mazishi baba mzazi wa marehemu,Bonifasi Mashamba alisema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanae na kuongeza kuwa aliishi na watu vizuri jambo lililochangia watu wengi kujitokeza kumuuguza ikiwa ni pamoja na misaada mbali mbali.
Naye Mjomba wa marehemu, Innocent Sigonda alisema marehemu alikuwa akisumbuliwa na kansa ya mapafu pamoja sukari ilikuwa ikishuka mara kwa mara.
Mwenyekiti wa tawi la Yanga mkoa wa Mbeya Lusajo Kifamba alisema marehemu alikuwa mwanachama wao hivyo uongozi unasikitika kumpoteza mwanachama wake ambaye alikuwa akitoa msaada wa kiufundi kila alipotakiwa.
Naye mwakilishi wa uongozi wa yanga makao makuu Shadrack Nsajigwa alisema marehemu aliishi naye kama ndugu kwani walisaidiana na kupeana ushauri.
Alisema marehemu alikuwa na kipaji cha mpira pia alikuwa anajituma hivyo alikuwa mfano wa kuigwa kwa vijana waliopo.
Aliongeza kuwa wachezaji wa zamani ni hazina kwa taifa hivyo ni vyema wakatunzwa na kuthaminiwa.
Aidha alitoa wito kwa wachezaji wengine kujipanga kimaisha ili baada ya kustafu wasisubiri kuomba misaada pindi wapatapo matatizo.
Alisema in vyema pia kuanzisha vyama vya kuwasaidia kama wachezaji wastaafu.
Social Plugin