MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa zuio la muda kuzuia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe asikamatwe na Polisi hadi maombi yake, aliyoyaomba ya kutaka asikamatwe, yatakaposikilizwa kesho.
Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe anapinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO), Camilius Wambura, ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Maombi ya kesi hiyo yataanza kusikilizwa Februari 23, mwaka huu saa 7:30 mchana katika chumba cha wazi cha mahakama ili kuruhusu watu mbalimbali kusikiliza kesi hiyo.
Jopo la majaji watatu likiongozwa na Sekieti Kihiyo akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday lilitoa zuio hilo, hata hivyo walisema Polisi wanaweza kumuita Mbowe kwa mahojiano pindi watakapomhitaji.
Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa kwa vipindi vitatu kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana, mahakama iliamuru upande wa wadai ambao uliongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kurekebisha maombi yao kwa kuwa hawakumuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) licha ya kuishitaki serikali.
Hali hiyo ilitokana na mawakili wa upande wa wadai, Lissu ambaye alipinga kitendo cha Mwanasheria wa Serikali, Gabriel Malata kuwatetea wadaiwa hao ambao ni RC, RPC na ZCO katika kesi hiyo kwa kuwa hawajaitaja serikali.
Akijibu hoja hiyo, Malata alidai kuwa waliofunguliwa madai hayo sio Makonda, Sirro wala Wambura, bali ni serikali hivyo ana mamlaka yote ya kuwawakilisha.
Baada ya pande zote kuwasilisha hoja zake, mahakama ilimruhusu Malata kuendelea kusikiliza kesi hiyo ambapo pia iliagiza upande wa wadai kufanya marekebisho ya maombi hayo na kumuongeza AG kama mdaiwa.
Hata hivyo, Lissu aliomba waruhusiwe kufanya marekebisho hayo kwa kumuongeza AG, ombi ambalo halikuwa na pingamizi.
‘’Tutafanya marekebisho ya maombi yetu na marekebisho mengine madogo madogo kwa namna tutakavyoona inafaa siku ya Jumatatu na tutawapa wajibu maombi Machi 6 mwaka huu na Machi 8 mwaka huu itatajwa kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo,’’ alidai Lissu.
Mbowe aliwasili mahakamani hapo akiwa na gari lenye usajili namba T 830 aina ya Land Cruiser, saa chache kabla ya kesi yake kuitwa katika chumba namba 64 kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alifika mahakamani hapo baada ya kutoka Kituo Kikuu cha Polisi saa 7 usiku, alikokuwa anahojiwa na kupekuliwa kuhusu sakata la dawa za kulevya.
Aidha, viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, madiwani na wafuasi wao walijitokeza kwa wingi, kusikiliza kesi hiyo huku wakifurahia amri ya mahakama ya kuzuia kutokamatwa kwa mwenyekiti huyo.
Katika kesi ya msingi, Mbowe anaomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni, pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba, itakapomalizika na kwamba polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu, iko kinyume cha katiba, kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.
Pia anadai kuwa kwa mazingira ya sasa, sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.
Mbowe pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.
Vile vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo, basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.
Kigwangalla acharuka Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla ameagiza ndani ya miezi sita, kujengwe vituo vya dawa ya kuacha utegemezi wa dawa za kulevya aina ya Methadone kila mkoa pamoja na vituo vya urekebishaji.
Aidha, Kigwangalla ameagiza pia ufanyike utanuzi wa vituo vilivyopo sambamba na kupatikana wataalamu watakaofanya kazi hizo.
Kigwangalla alisema pia kuwa serikali imebaini mkakati unaofanywa chini kwa chini wa kuwarudisha watu, ambao wameamua kuacha dawa za kulevya ambao wanatumia Methadone, kwa kuwaeleza kuwa dawa hiyo hazifai ambapo ameagiza wanaofanya hivyo wakipatikana washitakiwe.
Akizungumza baada ya kutembelea kituo cha Methadone na kuona namna kinavyofanya kazi pamoja na ufinyu wa eneo katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam jana, Kigwangalla alitoa agizo hilo kwa Katibu Mkuu (ambaye hakuwepo kwenye ziara hiyo) “Kila hospitali ya mkoa lazima iwe ya misheni au vipi, ni lazima ijenge, na itafute eneo jirani ijenge ‘rehabilitation center’, natoa miezi sita, na hii ifike kwa Katibu Mkuu Tamisemi pia,” alisema Kigwangalla.
Alisema wakati mamlaka nyingine zinadhibiti dawa za kulevya, sekta ya afya nayo inajipanga namna ya kutoa huduma nchi nzima. Hivi karibuni Tanzania imeingia katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ambapo Rais John Magufuli ameagiza mapambano haya yawe ya taifa zima.
Kigwangalla alisema mwaka huu wameongeza Methadone kutoka kilo 90 hadi 120. Kwamba bajeti ijayo, lazima iongezwe dawa hizo, kwani mikoa hiyo mingine itakua imeanza kutoa huduma.
“Kwa sasa hatuna namna kama kuna waathirika huko mikoani ni lazima waje katika vituo vyetu hapa Dar es Salaam mpaka tutakapokamilisha huduma huko mikoani, “ alisema.
Aliwataka pia kuangalia kama ni kuwasambaza madaktari bingwa wa afya ya akili waliopo, wapelekwe kila mkoa au kuajiri kama hawatoshelezi. Kigwangala ametoa pia miezi mitatu kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukiza nchini, kutafakari namna ya kuboresha kipato cha mtu ambaye anahudhuria kliniki ya dawa aina ya Methadone ili asishawishike kurudi katika janga hilo.
“Mteja huyu analazimika kusafiri kuja kituoni kupata dawa na kurudi, na anakua katika mazingira ambayo hawezi kuajirika kirahisi, hafanyi chochote inaweza kumsababishia arudi katika utumiaji wa dawa za kulevya,” alisema Kigwangalla.
Awali Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili na msimamizi wa kituo hicho, Cassian Nyandindi alisema kati ya changamoto zinazokabili kituo hicho ni waathirika kukosa shughuli za kuwaingizia kipato cha kuwasaidia katika maisha yao pamoja na nauli na pia uchache wa watoa huduma ambapo wapo madaktari wawili tu huku watu wanaohitaji huduma kwa siku ni zaidi ya 100.
Aidha, Naibu Waziri huyo aliagiza pia kuongezwa nafasi ya huduma, kwani eneo likilopo sasa katika hospitali hiyo halitoshi kama alivyoelezwa na Dk Nyandindi kwasababu serikali inatarajia ongezeko kubwa la waathirika kufurika katika vituo vya huduma ya methadone.
Alisema ni lazima kuanza kutafuta eneo la kuongeza vituo vyote kuongezewa nafasi ya kutosha.
Kigwangalla aliagiza pia kwa vyombo vya ulinzi kuweka ulinzi katika vituo hivyo kwani kuna taarifa kuwa wauzaji wa dawa za kulevya wanazungukia vituo hivyo kuwashawishi watumiaji wa Methadone warudi katika matumizi ya dawa za kulevya.
“Naagiza muwasiliane na jeshi la polisi waje kuweka kambi katika vituo hivi ili wawafuatilie wateja wa kliniki zetu wasirudishwe kwenye matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Kigwangalla.
Akifafanua alisema mtumiaji mmoja anatumia Sh 10,000 hadi 150,000 kwa siku ina maana kwa watumiaji wa methadone 3,351 waliopo katika vituo vya Dar es Salaam wamepunguza soko la dawa za kulevya.
“Maana yake ni kwamba tumeondoa sokoni kwa hawa wauza dawa za kulevya Sh bilioni 70, kwahiyo nao wanaangalia kutanua wigo wa soko lao kwa kuwarudisha watu hawa tunaowasaidia, “ alisema Kigwangala.
Alisema serikali sasa inapambana na hao wauza unga na atakayepatikana akiwashawishi vijana hao atajumlishwa kwenye kesi ya kuingiza, kusambaza na kuuza dawa hizo.
Alisema anatoa agizo pia kitengo cha uthibiti wa dawa za kulevya kiimarishwe na kuongezewa wataalamu wa afya ya akili wasiopongua watano ili kuendana na kasi hiyo.
Naibu Waziri huyo alisema pia kuwa yeye kama mtaalamu alisema dawa hiyo, inasaidia watu lisitokee kundi likapotosha kwamba dawa hiyo haisaidii.
“Mtu yeyote anayesema Methadone haisaidii muulize yeye amrsomea nini, mambo ya kitaalamu yanapingwa kwa hoja za kitaalamu na sio za kisiasa, unatakiwa ufanye utafiti na useme nini ni sahihi kwa takwimu,” alisema.
Alisema ziara hiyo inatokana na vita dhidi ya dawa za kulevya inayoendelea sasa nchini kuwasaidia waathirika kuwarudisha katika hali yao ya kawaida.
“Anapoanza matumizi anakua ni kwa ridhaa yake lakini kuacha anakuwa ni mgonjwa, sio kwa ridhaa yake kwa sababu anapoacha anakuwa kama kichaa anapata arosto ambayo anaweza kujidhuru, “ alisema Kigwangalla.
Mbinu mpya ya kusafirisha ‘unga’ Katika hatua nyingine, wauzaji na wasafirishaji wa mirungi wilayani Handeni wamebuni mbinu mpya ya kusafirisha shehena za dawa hizo, ambapo baada ya serikali kudhibiti njia zao, sasa wanatumia wanafunzi kama chambo cha kusafirisha dawa hizo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Handeni ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe imebaini kuwa mirungi hiyo husafirishwa kwa kutumia Pikipiki na hujazwa kwenye mabegi, ambayo nyuma anapakizwa mwanafunzi akiwa na sare za shule.
Mirungi ni miongoni mwa dawa za kulevya ambazo zinapigwa marufuku na Sheria ya Udhibiti wa Dawa ya Kulevya ya mwaka 2015, ambapo Kifungu cha 15(b) kinasema anayepatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya hukumu yake ni kifungo cha maisha.
Akizungumza na Habari Leo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe alisema kuwa wamebaini mbinu hizo baada ya kuendesha msako mkali na kufanikiwa kukamata kilo 88 za mirungi.
“Tumeunda timu ambayo Mwenyekiti wake ni OCD itakayokuwa inafanya doria usiku na mchana ili kuhakikisha vijana wetu wanabaki salama na kukomesha kabisa biashara ya madawa ya kulevya.”
Alisema Gondwe Alisema wafanyabiasha hao wa dawa za kulevya aina ya mirungi wamekuwa wakigawanya mirungi hiyo kwa kilo, kisha husindikizwa na vijana wenye silaha na pikipiki zao hupita karibu na shule za Sekondari ili kuwazuga Polisi kwa kuona kuwa ni wanafunzi wanapelekwa shule.
Baada ya kupita eneo hilo, pikipiki hizo huenda hadi katikati ya mji ambako mirungi hufungwa katika ujazo tofauti na kuuzwa rejareja na rumbesa ya mirungi aina ya colombo huuzwa Sh 8,000, wakati ya asili Sh5,000 na ile ya rungu huuzwa Sh 2,000.
“Ukitazama hizo pikipiki zikipita utadhani zinawapelekwa wanafunzi shule kumbe ndio zina mizigo, lakini tumebaini mbinu zao na wapo watu kadhaa ambao wanashikiliwa na jeshi la Polisi,” alisema.
Alisema Kamati yake itaendelea kushirikiana na jeshi la Polisi, Zimamoto na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kudhibiti biashara hiyo ya mirungi na bangi wilayani humo.
Gondwe alisema kuwa msako huo ni endelevu, kuunga juhudi za Rais John Magufuli katika kupiga vita dawa za kulevya. Alisema wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu, watakamatwa.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin