Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ameagiza kukamatwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Chidi Mapenzi ambaye ni mume wa msanii maarufu wa filamu nchini Shamsa Ford kwa ajili ya mahojiano kuhusu dawa za kulevya.
Makonda ametaja jina la Chidi Mapenzi leo wakati akihitimisha mkutano wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya vita dhidi ya dawa za kulevya katika mkoa wa Dar es Salaam, ambayo imeambatana na kukabidhi orodha mpya ya majina ya watuhumiwa wengine 97 kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dkt. Rogers William Sianga.
Mara baada ya kupokea majina hayo, Kamishna Sianga amesema kuwa atayashughulikia na atahakikisha kila mtu anakamatwa na kushughulikiwa bila kumuonea mtu kwa mujibu wa sheria iliyounda mamlaka hiyo.
Jina lingine lililotajwa leo ni Mfaume Kiboko, ambapo Kamishna Sianga ameagiza pia akamatwe na apelekwe kwake haraka iwezekanavyo.
Katika hotuba yake, Mh. Makonda pamoja na kuweka wazi kuwa moto wa vita hiyo ndiyo unaanza kuwaka sasa, amewaonya watu wote ambao wanakaidi amri yake ya kuripoti polisi na kuwatangazia vita zaidi, huku akisema yeye kama mkuu wa mkoa ana mamlaka yote ya kumuita mtu yeyote na ikiwezekana kumfukuza kwenye mkoa wake.
"Ukiitwa polisi nenda, hizi mbwembwe nyingine achana nazo, hizo mbwembwe siyo kwenye utawala huu wa Magufuli, na siyo kwenye utawala na Makonda, Mwingine anasimama kabisa na kifua chake eti hawezi kwenda kwa sababu eti Makonda ni kijana mdogo, sasa kama Makonda ni mdogo hawezi kukuita wewe, atapajua shimoni ni wapi, Pia nina mamlaka ya kukufukuza kwenye mkoa wangu endapo nitajiridhisha kuwa wewe ni hatari kwenye mkoa wangu" Amesema Makonda
Makonda amesema atatumia sheria mpya ya mwaka 2015 kuwashughulikia wote wanaohusika bila kujali ni nani, na kufafanua kuwa sheria hiyo inaelekeza pia adhabu kwa watumiaji na kuwataka watu wanaokosoa uamuzi wake wa kutaja majina waungane naye, kwa kuwa wao ndiyo waliotaka majina hayo awali
"Sheria mpya ya mwaka 2015 inasema mtumiaji wa dawa za kulevya atafungwa jela miaka mitatu, kuna wengine hakuna sheria ya kumuadhibu mtumiaji, hawahui sheria........Kuna wengine wakati ule wa Kikwete, aliposema ana majina walitaka ayataje, sasa leo Makonda anataja wanaanza kelele, nale ninayo majina mengine 97, na haya ndiyo yana watu wazito zaidi, na yataleta mtikisiko zaidi"
Pia ametaja baadhi ya mbinu mpya ambazo hutumiwa na wasambazaji wa dawa za kulevya kuwa ni pamoja na kutumia mitungi ya gesi, pamoja na kuwatumia wauza vitumbua mitaani.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Simon Sirro, amesema tangu Februari 01 hadi 12 mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 311 wamekamatwa na kuhojiwa wakiwemo 77 waliotajwa na Makonda.
Amesema kati ya hao 311, watuhumiwa 117 walikutwa na vielelezo.
Social Plugin