Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAUL MAKONDA AJILIPUA DAWA ZA KULEVYA

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amejitoa mhanga kwa kuagiza kuswekwa ndani kwa askari Polisi zaidi ya tisa wa mkoa huo pamoja na kuwataka wasanii maarufu nchini akiwamo aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi, akiwatuhumu kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mbali na Wema ambaye alikuwa Miss Tanzania 2006 na kwa sasa ni mwigizaji maarufu, Makonda akawataka wasanii wengine maarufu kujisalimisha leo katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, wakiwemo Khaleed Mohamed (TID), Winfrida Josephat (Recho), Khery Sameer (Mr Blue), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu) na Rashid Makwiro (Chid Benz).

Makonda anakuwa kiongozi wa kwanza nchini kujitokeza hadharani na kutaja wahusika au watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya kwa majina, baada ya miaka mingi wanasiasa kuishia kueleza kuwa wanayo majina ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu yenye fedha nyingi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Makonda aliwataja askari hao kwa jina moja moja ambao ni Swai, Neri, Willy, Mkomeo wote wa Kituo cha Polisi Oysterbay, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, Inspekta Fadhil wa Kinondoni, Steven wa Kinondoni, James wa Kinondoni, CP Dotto wa Kituo cha Kijitonyama na WP Glory wa Kituo cha Kawe.

Mkuu wa mkoa huyo pia amewataka wamiliki wenye leseni za kuendesha sehemu za starehe ambazo zinasadikika kujihusisha na uuzaji wa dawa hizo, kujisalimisha leo saa tano katika Kituo Kikuu cha Polisi wakiwemo wamiliki wa George Dragon, Element na Cuba Bar.

Makonda ambaye kabla ya uteuzi wake aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, aliwaambia waandishi wa habari kwamba amefikia hatua hiyo baada ya kufanya msako wa kuwakamata wahusika wa dawa za kulevya katika mkoa huo na baadhi ya wananchi kuwataja askari hao kuwa wanahusika kuwaficha wauzaji wa dawa hizo.

Alisema baada ya msako, wananchi walikuwa wanawataja wahusika wa dawa hizo, lakini polisi hawawajui ndipo alipopata taarifa kuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, jambo linalofanya kushindwa kutokomeza dawa hizo katika mkoa huo.

“Kwa mamlaka niliyonayo nataka wakamatwe kama wapo ndani ya mkoa au nje waletwe na wawekwe mahabusu pale Central, watoe maelezo kwa nini wananchi wanawataja, kuna wengine wanatajwa kuwapigia simu wahusika wakati wakienda kuwakamata na wanatumiwa hela kupitia simu zao, hizi ni tuhuma na wao wana nafasi ya kujieleza,” alisema Makonda.

Aidha, Makonda aliwataja baadhi ya watu wanaosadikika kuwa ni wafanyabiashara wa dawa hizo ambao tayari wameshakamatwa akiwemo Ahmed Ngahemela (Pettit man), Said Lina maarufu kama Alteza, Nassoro Nassoro, Bakari Khelef pamoja na Omary.

“Wapo wengi, lakini hawa ndio tayari tumewakamata na wengine wamekutwa na dawa hizo, tunaendelea na msako ambao nitauendesha mimi mwenyewe nikishirikiana na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, lengo ni kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya katika mkoa huu inatokomezwa,” alifafanua Makonda.

Makonda pia ametoa siku saba kutokomezwa kwa vijiwe na maeneo yote yanayojihusisha na uuzaji dawa za kulevya katika mkoa huo.

“Mnafahamu nipo na Kamishna Sirro na kamati yake baada ya siku saba nitawaambia kama watashindwa kutokomeza dawa za kulevya Dar es Salaam maana yake wamekosa sifa za kuendelea kuwa askari katika mkoa wetu, kwa kuwa wameshindwa kuwafahamu wauzaji,” alibainisha Makonda.

Naye Kamanda Sirro alisema atalizungumzia hilo kwa waandishi wa habari atakapokutana nao leo.

IMEANDIKWA NA SOPHIA MWAMBE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com