Mchungaji Anthony Lusekelo amefunguka kuhusu tuhuma za yeye kunywa pombe, na kuweka wazi kuwa hanywi pombe bali anakunywa 'wine' isiyo na kilevi, huku akisita kusema endapo unywaji pombe ni dhambi au siyo dhambi.
Amefunguka hilo alipokuwa kwenye kipindi cha KIKAANGONI cha EATV, na kuweka wazi kuwa wanaomtuhumu kuwa yeye anakunywa pombe wanapaswa kutoa ushahidi juu ya tuhuma hizo, na kwamba unywaji pombe unaweza kuwa dhambi ama usiwe dhambi kulingana na imani na dini ya mtu.
"Hao wanaotuhumu kuwa nakunywa pombe, waeleze ni pombe gani nakunywa, nilikuwa nakuywa wapi na aliyeniona ni nani... kuna sehemu nyingine pombe siyo dhambi, dini nyingine mpaka kanisani kuna bar".
Je, kunywa bia kiasi bila kulewa ni dhambi au siyo dhambi?
Hilo ni swali lingine alilokutana nalo kuhusu unywaji Pombe, ambapo katika majibu yake amesema hawezi kusema kama ni dhambi au lah, maana inategemea na imani ya mtu, huku akiongeza kuwa Bibilia haijazuia unywaji pombe
"Inategemea na makanisa, kuna mengine hata kunywa soda ni dhambi. Dhambi ni makubaliano yenu kwenye dini yenu. Bibilia inasema kula kitu chochote hata chakula kama ukila kupitiliza ni dhambi, hata unywaji wa pombe ukinywa ukapitiliza ni dhambi. Biblia haijaandika moja kwa moja kwamba msinywe pombe, imesema msilewe kwa kuwa ndani ya ulevi kuna ufisadi, cha msingi mbadilishe ulevi wenu uwe ni roho mtakatifu"
Ikumbukwe kuwa sekeseke lililosababisha Mzee wa upako adaiwe kunywa pombe, lilihusisha kurushiana maneno na jirani zake ambapo baada ya hapo vyombo vya habari hasa magazeti yaliripoti tukio hilo kwa namna ambayo Mzee wa Upako hakuipenda, na hata kufikia hatua ya kuwatabiria kifo waandishi walioandika habari hiyo.
Alipoulizwa kuhusiana na ahadi yake hiyo ya kuwatabiria vifo, alisema kuwa tayari amewasamehe ingawa uwezo wa kuwaombea kifo anao.
"Tulisema hatuwezi kutumia nguvu kubwa sana kuwaombea watu kifo, kwa sababu sisi ni wanadamu, na wanadamu tuna mapungufu kwahiyo nikaona ni bora kumuachia Mungu. Uwezo huo wa kuwaombea watu wakafa, mimi ninao, lakini nikaona inasaidia nini mtu kumuombea mabaya, kwahiyo nikaamua kusamehe"
Baadhi ya watu walitaka kujua ni kwanini haendi kuombea wagonjwa hospitalini ili wapone, ambapo alijibu kuwa maombi hufanywa katika mazingira maalum, na kwamba hospitali kila mgonjwa ana imani yake.
"Maombi lazima kuandaa mazingira, na sehemu ambayo Mungu amesema tukutane ni kanisani, ndiyo maana hata wakati wa Yesu wagonjwa ndiyo walimfuata Yesu, siyo Yesu aliwafuata wagonjwa.. Kinachoponya ni imani ya mtu, pale hospitali kila mtu ana imani yake, wakati mwingine hata kumuombea mtu inabidi umuombe kwanza maana wengine hawapendi kuombewa"
Social Plugin