NI mechi ya vita na kisasi. Ndivyo ambavyo inaweza kutafsiriwa katika mchezo wa mahasimu wawili Simba na Yanga utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni vita kwasababu ndizo timu zinazoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa tofauti ya pointi mbili, Simba ikiwa na pointi 51 katika michezo 22 na Yanga ikishika nafasi ya pili kwa pointi 49 katika michezo 21 iliyocheza.
Aidha, Simba ina ukame wa mataji ya ligi baada ya kukosa karibu misimu minne ikizidiwa na Yanga ambao ni mabingwa watetezi wakishinda taji hilo karibu misimu mitatu mfululizo.
Simba ambao ndio wenyeji wanahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kubaki kileleni na kutetea nafasi yao ya uongozi na kuwa rahisi katika mbio za kusaka ubingwa. Pia, Yanga wanahitaji ushindi kuwa katika nafasi nzuri ya kutetea taji lao.
Ni mchezo ambao utatoa taswira nani akayechukua ubingwa msimu huu ndio maana vita lazima iwepo ya kuwania kupata pointi tatu kwa kila mmoja.
Pia, ni mchezo wa kisasi kwa vile Simba imeshindwa kutamba mbele ya Yanga baada ya raundi ya kwanza kutoka sare ya bao 1-1. Pia, msimu uliopita Simba ilifungwa jumla mabao 4-0, kwa maana ya raundi ya kwanza 2-0 na ya pili 2-0.
Kwa ujumla, michezo waliyowahi kucheza ni 92 na kati ya hiyo, Yanga imeshinda 35 na Simba 25 wakipata sare 32, Yanga ikiongoza kwa magoli 101 na Simba 89.
Katika ligi msimu huu mpaka sasa, Yanga inaongoza kwa mabao 46, Simba 36 hivyo kuonesha wazi kuwa wako vizuri katika safu ya ushambuliaji.
Katika mabao ya kufungwa Yanga imefungwa tisa na Simba saba, hivyo wekundu hao wa Msimbazi wako vizuri katika safu ya ulinzi. Katika safu ya ushambuliaji, Yanga inawategemea Simon Msuva, Obrey Chirwa na Amis Tambwe.
Pia, Donald Ngoma ingawa uongozi wa Yanga ulisema unamwandaa kwa ajili ya mchezo wa kimataifa dhidi ya Zanaco. Simba inawategemea Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya katika mashambulizi.
Timu hizo zote zinaongozwa na makocha wa kigeni wenye uwezo wa kusoma mchezo na kufanya mabadili ya maana ili kupata matokeo.
Simba ikiwa na Joseph Omog mwenye uzoefu na mechi hizi tofauti na George Lwandamina ambaye utakuwa ni mchezo wake wa kwanza wa ligi kukutana na mahasimu hao ukiacha ule wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar walipotoka sare ya bila kufungana.
Huu utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa Lwandamina kukutana na mechi yenye presha ya mashabiki wengi uwanjani.
Mechi hii inatarajiwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati Mathew Akrama kutoka Mwanza akisaidiana na Mohamed Mkono wa Tanga na Hassan Zani wa Arusha.
Huyu ni mwamuzi ambaye hana beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), lakini amechaguliwa kutokana na aina ya mechi hii yenye presha, kutokana na uadilifu kwamba anaweza kuchezesha kwa haki kama ambavyo inatarajiwa na wengi.
NA GRACE MKOJERA
Social Plugin