Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA VIONGOZI MBALIMBALI IKULU DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 17 Februari, 2017 amekutana na Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati Bw. Amadou Hott ambaye yupo hapa nchini kwa mazungumzo na wataalamu na viongozi yenye lengo la kuboresha sekta ya nishati hususan uzalishaji wa umeme.

Bw. Amadou Hott amekuja nchini ikiwa ni utekelezaji wa mazungumzo yaliyofanywa kati ya Mhe. Rais Magufuli na Rais wa AfDB Bw. Akinwumi Adesina Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 31 Januari, 2017 ambapo viongozi hao walikubaliana kuongeza ushirikiano kati ya AfDB na Tanzania katika maendeleo huku mkazo ukielekezwa kupata majawabu ya kuongeza uzalishaji wa umeme na wa gharama nafuu.

Bw. Amadou Hott ameelezea kuguswa na dhamira ya Mhe. Rais Magufuli juu ya kuongeza uzalishaji wa umeme na wenye gharama nafuu kwa ajili ya kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, na ameahidi kuwa Benki hiyo itahakikisha dhamira hiyo inafanikiwa.

Kwa Upande wake Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Bw. Amadou Hott kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote itakapohitajika ili kufanikisha dhamira hiyo.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bharti Enterprises inayomiliki kampuni ya simu ya Airtel Duniani Bw. Sunil Bharti Mittal ambapo viongozi hao wamezungumzia utendaji kazi wa kampuni ya simu ya Airtel Tanzania ambayo Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo, Bw. Sunil Bharti Mittal ameelezea utayari wake wa kuingiza kampuni ya Airtel Tanzania katika soko la hisa la Dar es Salaam ili Watanzania wapate fursa ya kumiliki kampuni hiyo kwa kununua hisa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hapa nchini Mhe. Jean Pierre Tshampanga Mutamba Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais , IKULU
Dar es Salaam
17 Februari, 2017

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com