Rais Magufuli ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata wanaohusika na Dawa za Kulevya bila kuangalia umaarufu au cheo cha mtu.
Magufuli ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Vanance Mabeyo pamoja na viongozi wengine wa majeshi, na mabalozi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alianza kwa kumpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kwa hatua nzuri aliyoichukuwa ya kuwasimamisha kazi Askari Polisi 12 waliotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya ili kupisha uchunguzi.
Rais Magufulia amesema hakuna wa kuachwa hata akiwa mkewe Mama Janet Magufuli, na kuongeza kuwa wakamatwe bila ya kujali majina yao.
"Najua IGP Mangu watu walikupigia simu wanakupa ushauri kuhusu Dawa za Kulevya, ungewasikiliza leo usingekuwa IGP.
"Vita ya dawa za kulevya haina cha umaarufu, haijalishi ni mtoto wa nani anahusika, hata kama ni mke wangu mkamateni.
"IGP nakuagiza kamata watuamiaji wote wa dawa za kulevya hao watakwambia wanapozipata, haiwezekani ziuzwe kama njugu",amesema Rais Magufuli
Akizungumzia suala la uendeshaji wa kesi za dawa kulevya, Rais Dkt Magufuli amemwambia Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa kesi hizo zinaendehswa taratibu sana huku akitolea mfano wa mfanyabiashara mmoja maarufu wa dawa za kulevya aliyekamatwa mkoani Lindi lakini hakuwahi kufikishwa mahakamani.
"Kuna mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya alikamatwa mkoani Lindi lakini sijawahi kusikia amefikishwa mahakamani" Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa vita ya dawa za kulevya si ya Paul Makonda peke yake bali ni ya Watanzania wote huku akivitaka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kushirikiana kutokomeza tatizo hili linalopelekea kupoteza nguvu kubwa ya taifa.
Kauli hii ya Rais Magufuli inakuja ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda atangaze vita dhidi ya watu wanaohusika na dawa za kulevya akianza kwa kutaja majina yakiwemo ya askari na ya wasanii maarufu wa muziki na filamu akiwemo Wema Sepetu, Chid Benz, Vanessa Mde n.k.
Siku tatu baada ya Makonda kuwataja watuhumiwa hao, IGP Ernest Mangu alichukua hatua ya kuwasimamisha askari 12 waliotajwa na kuahidi kuchukua hatua zaidi, jambo ambalo limepongezwa na Rais Magufuli na kumueleza kuwa endapo asingechukua hatua hiyo, angejua kuwa na yeye anahusika.
Social Plugin