Serikali imevifuta vituo vyote vya taasisi zisizo za kiserikali vinavyotoa huduma za afya ya VVU na Ukimwi, kwa makundi maalum kutokana na kubainika kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja.
Baada ya kuvifuta, serikali imeelekeza huduma hizo sasa kutolewa tu kwenye vituo vya umma pamoja na vituo vya afya vya binafsi vilivyosajiliwa.
Tamko hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambapo amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo kutokana na maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa makundi maalum kuongezeka ikilinganishwa na wastani wa kiwango cha maambukizi nchi nzima.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Prof. Muhammad Bakari Kambi amesema katazo hilo limelenga kupunguza maambukizi ya VVU na Ukimwi ambayo kwa sasa yameongezeka.
Wakati huo huo Waziri Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kubadilisha kadi za homa ya manjano za zamani na kupatiwa kadi mpya na kusisitiza kuwa kuanzia tarehe 31 Machi mwaka huu kadi za zamani za homa ya manjano hazitatumika na kueleza gharama ya kubadilisha ni Shilingi 500 kwa Mtanzania na dola 10 kwa raia wa nje.
Social Plugin