Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIGOGO WANNE WA SHIRIKA LA POSTA WATUMBULIWA KWA WIZI NA UMANGIMEZA


BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, imetengua nafasi tatu za mameneja na ofisa mwandamizi kutokana na vitendo vya umangimeza, urasimu, kufanya kazi kwa mazoea, ubadhirifu na wizi.

Mameneja waliotenguliwa ni James Sando ambaye alikuwa Meneja Mkuu, Menejimenti ya Rasilimali. Macrice Mbodo ameteuliwa kushika nafasi hiyo.

Mwingine aliyetenguliwa ni Meneja Mkuu Uendeshaji wa Biashara Janeth Msofe. Aliyekuwa Meneja wa Mkoa Shinyanga, Hassan Mwang'ombe kateuliwa kushika nafasi hiyo.

Bodi pia imewasimamisha kazi Meneja Msaidizi wa Barua na Logistic, Jasson Kalile na Ofisa Mwandamizi wa Usafirishaji, Ambrose John.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Dk. Haruni Kondo, ameyasema hayo wakatia akizungumza na waandishi wa habari kuwajulisha uamuzi uliofanywa na bodi.

Dk. Kondo amesema, imebainika na imewaridhisha kuwa baadhi ya watendaji wakuu wa makao makuu ya Posta wamekuwa kikwazo katika dhana ya uwajibikaji, weledi na kujituma katika kutekeleza wajibu na majukumu yao, ili kulifanya shirika hilo kuwa mfano bora wa mashirika yenye ubora katika kutoa huduma.

Ametoa mfano wa mkataba wenye utata wa kukodisha magari ya kusafirisha barua kuwa kukodisha magari kwa siku inalipwa Sh. milioni 10, kwa wiki Sh milioni 70 na kwa mwezi Sh. milioni 300.

Amesema, mkataba huo haufai na mmoja wa waliousaini amewajibishwa.

"Kuna vitendo vya baadhi ya watendaji vinadhihirisha tabia ya umangimeza, urasimu, kufanya kazi kwa mazoea, ubadhirifu na wizi," amesema.

Kondo amesema, baada ya bodi kufanya tathmini yake kuhusu utendaji wa wafanyakazi wa shirika, ilielekezwa menejimenti ichukue hatua kwa kada zote za wafanyakazi kuanzia Makao Makuu, Zanzibar, mikoani, wilayani hadi vijijini.

IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI- HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com