Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene amesema kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Simbachawene ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Chemba Juma Nkamia kuhusu Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwa wababe katika maeneo yao ya kazi.
“Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanasimamia maeneo yao kwa mujibu wa sheria na wana haki ya kuwachukulia hatua watumishi ambao hawatekelezi majukumu waliyopewa,” alifafanua Simbachawene.
Aliendelea kwa kusema kuwa, hata kama kuna Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni wababe katika maeneo yao ya kazi hauwezi kusema kila Mkuu wa Mkoa au Wilaya aliyechukua hatua dhidi ya mtumishi ambaye hawajibiki katika kazi yake ni mbabe au muonevu.
Aidha, Simbachawene amesema kuwa ni wakati sasa wa watumishi wa Umma kutekeleza wajibu wao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Kwani hakuna kiongozi ambaye ataweza kumchulia hatua mtumishi ambaye anawajibika na kazi zake kama alivyopangiwa.
Vile vile amesema kuwa, wakuu hao wa Mikoa na Wilaya wamekuwa wakifanya kazi nzuri katika maeneo wanayoyasimamia, kutokana na watumishi wengi wa Serikali walikuwa wamejisahau kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kimazoea.
Social Plugin