Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU AAGIZA MADIWANI WASIMAMIE MAKUSANYO YA FEDHA KWENYE HALMASHAURI ZAO


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema madiwani wanao wajibu wa kusimamia makusanyo ya fedha kwenye halmashauri zao na ametaka wakuu wa idara wawape taarifa kila inapobidi.

Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa umma wa Wilaya ya Mbulu kwenye kikao kilichofanyika katika Hospitali ya Haydom mkoani Manyara.

Waziri Mkuu ambaye amejiwekea utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma katika kila halmashauri kila anapofanya ziara mikoani. Amesema anafanya hivyo ili kuwakumbusha watumishi wajibu walionao wa kuwatumikia wananchi ambao wameichagua na kuiweka serikali madarakani.

“Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na watumishi wa chini na ndiyo maana katika ziara zangu nimeweka ratiba ya kukutana na watumishi wa umma ili kuwapa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwahudumia Watanzania,” amesema.

“Nimekuja kuwasisitiza watu wafanye kazi na Mheshimiwa Rais Magufuli anataka watumishi wafanye kazi ya kuwahudumia Watanzania bila ubaguzi. Msiwabague watu kwa uwezo wao wa kifedha, itikadi za siasa au kwa rangi zao,” amesisitiza.

“Tunataka muwahudumie wananchi kwa umahiri kila mmoja katika sekta yake. Hatutaki kusikia kauli za ‘njoo kesho’, ‘njoo kesho’ kwa sababu inajenga nafasi ya rushwa. Tunapambana na wala rushwa kwa sababu wametupotezea fedha nyingi ambazo zingetumika kuwahudumia wananchi kwenye miradi ya maji au miradi mingine ya maendeleo,” amesema.

Amesema jambo kubwa ambalo anawasisitizia watumishi hao ni uadilifu na uaminifu, kwani serikali hivi imeamua kuleta fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo na inatarajia fedha hizo zitatumika kule zilikopangiwa.

“Fedha za maendeleo ziende kutumika kwenye miradi iliyopangwa. Fedha hizi msiziguse kwa sababu zina moto. Mtumishi yoyote ukizichezea zitakuunguza. Kuweni makini na hizi fedha,” alisisitiza, na kuongeza kuwa wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa idara washirikiane na madiwani na wawajulishe kila mara wanapopokea fedha kutoka Serikali Kuu. “

“Ni lazima muwajulishe kuwa mmepokea fedha kiasi gani na zimekuja kwa ajili ya kazi gani mahususi. Wao kwa mujibu wa madaraka yao, ni wasimamizi wa hizi fedha. Hakikisha wanapata taarifa na ili kurahisisha mawasiliano, wakuu wa idara mkipata fedha hizi ni lazima muwajulishe wasaidizi wenu ili wajue nini kinaendelea. Ushirikishwaji ni kitu cha muhimu kwenye halmashauri zetu. Mkipata mafanikio wajulisheni pia madiwani wenu ili wakawasemee kwa wananchi,” alisisitiza.

Akitoa mfano kuhusu mtiririko wa fedha kwenye halmashauri, Waziri Mkuu alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu iliomba Sh milioni 203.6 kwa ajili ya kununulia dawa na mpaka sasa serikali imekwishatuma Sh milioni 175.

Akifafanua kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu alisema serikali inajali maslahi ya watumishi na kwamba imeanza kulipa madeni ya nyuma ambapo walimu zaidi ya 63,000 wamelipwa Sh bilioni 29 na watumishi wa kada nyingine wamelipwa kiasi cha Sh bilioni 21.

Amesema serikali pia imedhibiti malimbikizo ya watumishi yaliyotokana na likizo, kupanda madaraja, kupitia mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao umewezesha kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.

Mfumo huo unajulikana kama LAWSON. Ameisema mfumo huo ambao unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa umesaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hata anapostaafu.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com