Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AGPAHI YAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA KIFUA KIKUU – MERERANI MKOA WA MANYARA

Shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limeungana na wadau wote duniani katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani, 24 Machi 2017.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika mji mdogo wa Mererani, wilaya ya Simanjiro katika Mkoa wa Manyara, eneo ambalo Shirika la AGPAHI linatekeleza mradi wa kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI sehemu za migodini kwa hisani ya shirika la ADPP la Msumbiji.

Katika maadhimisho hayo, shirika la AGPAHI kwa kushirikiana na timu ya afya ya wilaya walifanya zoezi la kutoa huduma mbalimbali kwa jamiii inayozonguka mji mdogo wa Marerani kuanzia tarehe 23 – 25 Machi, 2017. 

Huduma zilizotolewa ni uchunguzi wa kifua kikuu, kupima Virusi vya Ukimwi na kutoa elimu kwa umma kuhusu kifua kikuu na VVU/UKIMWI.

Zoezi hilo lilisimamiwa na afisa mradi wa kifua kikuu na UKIMWI, kutoka AGPAHI, mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Simanjiro, wataalamu wa maabara, watoa huduma wa Afya kutoka kituo cha Afya Mererani na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani ni; “TUUNGANE PAMOJA KUTOKOMEZA KIFUA KIKUU”.

Shirika la AGPAHI linafanya kazi katika mikoa sita ambayo ni Mwanza, Geita, Mara, Tanga Shinyanga na Simiyu. Huduma zitolewazo na shirika la AGPAHI ni kusaidia serikali kupitia vituo vya kutolea huduma za afya katika:

1.Kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu 
wanaoishi na virusi vya UKIMWI; 

2.Kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya virusi vya 
UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto; 

3.Kutoa huduma ya uchunguzi wa dalili za awali na 
huduma za awali za saratani ya mlango wa kizazi
na 

4.Kutoa huduma shirikishi za kifua kikuu na UKIMWI
sehemu za migodini.

Vilevile, shirika linafanya kazi katika mji mdogo wa Mererani katika kutekeleza mradi wa kifua kikuu sehemu za migodini.

Matukio katika picha.
Afisa mradi wa Kifua kikuu na UKIMWI kutoka AGPAHI, Bi Alio Hussein akiwaelimisha na kugawa vipeperushi kwa wakazi wa Mererani kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI.
Mhudumu wa afya ngazi ya jamii akiwaelezea wakazi wa Mererani dalili za Kifua Kikuu na namna ya kuweza kujikinga na maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii wakichukua maelezo ya baadhi wakazi wa Mererani waliokua tayari kuchunguzwa kama wana maambukizi ya vijidudu vya Kifua Kikuu.
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Kajolii Maasai akitoa burudani na kuendelea kuwahimiza wakazi wa Mererani kuja kupata Elimu kuhusu Kifua Kikuu.
Elimu kwa wachimbaji wa madini ya Tanzanite kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI ikiendelea. 
Wachimbaji wa madini ya Tanzanite katika Kitalu D, wakiwa wamekusanyika kwa wingi wakielimishwa kuhusu Kifua kikuu na VVU/UKIMWI.
Bi. Alio Hussein akiwaonesha kwenye picha namna ambavyo vijidudu vya Kifua Kikuu vinaweza kusambaa kama mgonjwa atakohoa bila kuziba mdomo.
Wachimbaji wakielimishwa kuhusu aina za Kifua 
Kikuu kwa njia ya bango.

Maswali mbalimbali yakiulizwa kwa wachimbaji juu ya kifua kikuu na UKIMWI. 
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Kajolii Maasai akitoa burudani kwa wachimbaji wa Kitalu D waliokusanyika kwa wingi kuja kupata Elimu kuhusu Kifua Kikuu. 
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite akijibu swali lililoulizwa ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu Kifua kikuu na Ukimwi. 
Wa kwanza kushoto ni Kajolii Maasai msanii wa muziki wa kizazi kipya, wa pili kushoto ni mchimbaji wa madini ya Tanzanite ambaye alijishindia Tishirt baada ya kujibu vizuri swali kuhusu Kifua kikuu na watatu kutoka kushoto ni Afisa mradi wa Kifua kikuu na UKIMWI, Bi Alio Hussein, na mwisho ni Mratibu wa Kifua kikuu na Ukoma Wilaya ya Simanjairo, Bi Selestina Rosai.
Picha ya pamoja katika maadhimisho ya kifua kikuu - Mererani.

Na Joshua Fanuel wa Kilimanjaro Official blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com