Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AUAWA KISHA KUBURUZWA KWENYE PIKIPIKI KWA WIZI WA PIKIPIKI



KIJANA anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 ameuawa kwa kupigwa na wananchi, kisha kufungwa kamba miguuni na kuburuzwa kwenye pikipiki baada ya kutuhumiwa kuiba pikipiki.

Tukio hilo ni la Machi 6 saa 8 mchana katika Mtaa wa Kimondorosi, Kata ya Olasiti jijini Arusha na watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa kuhusika na mauaji ya mtuhumiwa huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema maelezo ya dereva wa bodaboda, mkazi wa Olasiti, Mtaa wa Kanisani aliyekuwa anaendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 349 BMW aina ya Toyo Power King, ni kwamba Machi 6, mwaka huu majira ya saa nane akiwa `kijiweni kwake’ kwa Mromboo alifuatwa na kijana anayemfahamu kwa sura na kumwambia ampeleke maeneo ya Kimondorosi Olasiti.

Alisema walipofika maeneo ya mlimani Mtaa wa Zambi, ghafla alikatwa sime shingoni na kwenye mkono wake wa kulia na abiria huyo wakati pikipiki ikiwa kwenye mwendo hali iliyosababisha kuanguka huku abiria huyo akichukua pikipiki na kutokomea nayo.

Alisema wakati abiria huyo alipokuwa akiondoka na pikipiki, mwanamke mmoja alishuhudia tukio hilo na alipiga kelele kuomba msaada na ndipo waendesha bodaboda na wananchi wa eneo hilo walishirikiana kumfukuza kijana huyo na kufanikiwa kumkamata akiwa na pikipiki hiyo aliyokuwa ameiiba.

Kamanda alisema watu hao walioamua kuchukua sheria mkononi na kumshambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kisha kumfunga miguu yote miwili kwenye pikipiki aliyoipora na kumburuza kwenye barabara ya lami kutoka eneo la Kwa Mrombo kwenda katikati ya mji.

Chanzo-Habari leo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com