Mahakama Kuu ya Tanzania leo Machi 2, 2017, imetoa uamuzi wa pingamizi la Serikali dhidi ya maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Freeman Mbowe aliyeiomba Mahakama ilizuie Jeshi la Polisi kumkamata akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Mbowe alifungua kesi ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Mkuu wa Upelelezi kanda maalum na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jopo la majaji wakiongozwa na Jaji Sekieti Kihiyo wameutaka upande wa mleta ombi hilo kufanyia marekebisho ya kifungu kwenye maombi ya Freeman Mbowe kuzuia kukamatwa na Jeshi la Polisi na kumuweka ndani wakati kesi ya msingi ikiendelea
Baada ya uamuzi huo, kiongoz wa jopo la mawakili wa upande wa Freeman Mbowe, Jeneral Ulimwengu alisema nje ya Mahakama baada ya maamuzi hayo kuwa,
“Ombi limekataliwa kwa sababu hatukuwa na kifungu ambacho katika sheria zetu kinafanya kazi katika nchi na maelekezo hayo ni kwamba kwa sababu tuna ‘import’ sheria zetu kutoka Uingereza. Tutafute kifungu ambacho kinaweza kusaidia kuendesha mashtaka, hiyo kazi itafanyika kati ya leo au kesho kwa sababu kesi ya msingi bado ipo na itasikilizwa March 8.” alisema Jenerali Ulimwengu.
Naye Mweneyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe baada ya maaamuzi hayo ya Mahakama alisema jopo la mawakili litahamia mjini Arusha kwenye kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha mjini (CHADEMA) Godbless Lema.
Social Plugin