MBUNGE WA CCM ASUSA AKIPINGA PIKIPIKI


MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) amelazimika kutoka katika kikao cha baraza la madiwani, ikiwa ni hatua yake ya kupinga Kaimu Mtendaji wa kata ya Kipili, Justine Jordan, kukabidhiwa zawadi ya pikipiki akitaka chombo hicho cha usafiri kiwe mali ya serikali na si ya mtu binafsi.

Tukio hilo lilitokea kabla ya kuahirishwa kwa baraza hilo la madiwani lililoketi katika Mji wa Namanyere, wilayani Nkasi wakati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Sumuni Mwanakulya alipokuwa akimkabidhi Jordan pikipiki aina ya SNLG namba MC 611BNP ya thamani ya zaidi ya Sh milioni mbili.

Jordan ambaye pia ni Ofisa Ugani alizawadiwa na halmashauri ya wilaya hiyo pikipiki hiyo baada ya kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kata yake.

Alikusanya zaidi ya Sh milioni 50 kati ya Sh milioni 100 alizopangiwa.

Mwenyekiti Mwanakulya alipolitangazia baraza hilo la madiwani kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imeamua kumzawadia Jordan pikipiki hiyo, baadhi ya madiwani walihoji uhalali wa zawadi hiyo wakitaka isiwe mali ya mtu binafsi bali iwe mali ya serikali.

Kutokana na hali hiyo, mbunge Keissy alisusa tukio hilo kwa kutoka ukumbini.

Mwanakulya alisisitiza kuwa halmashauri imemzawadia pikipiki hiyo Jordan na inakuwa mali yake huku akiwataka madiwani wasiwe na roho za kwa nini.

“Huyu mtendaji ametukusanyia zaidi ya Sh milioni 50 kati ya Sh milioni 100 aliyopangiwa, kumzawadia pipikipi ya thamani ya Sh milioni mbili imekuwa nongwa, hivi hizi roho za kwa nini zinatokea wapi? Pikipiki hii ni mali yake binafsi,” alisisitiza.

Pamoja na mjadala kuibuka ukumbini kwa baadhi ya madiwani kutokubaliana na hatua ya mtendaji huyo kupewa pikipiki, madiwani wengine walimmwagia Jordan sifa kwa kuweza kuvunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kata yake ya Kipili kwa uaminifu huku wakiwataka wengine waige mfano wake.

Akichangia, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo aliwakumbusha madiwani hao kuwa uamuzi wa kumzawadia Jordan pikipiki hiyo ulifikiwa katika vikao halali vya halmashauri hiyo.

Jordan licha ya kuishukuru halmashauri hiyo alisema kuwa mafanikio yake hayo yanatokana na yeye kuzingatia sheria na viwango vya ukusanyaji wa mapato ya ndani.

“Nilikuwa naamka usiku wa manane nawaomba wenzangu wajitume, kazi hii ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ina lawama nyingi ila wasiogope kutekeleza majukumu yao,” amesema Jordan.

IMEANDIKWA NA PETI SIYAME- habarileo NKASI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post