MKAZI wa Kijiji cha Tatanda kilichopo katika Kata ya Sopa wilayani Kalambo katika Mkoa wa Rukwa, Winfrida Mlungu (52), amekufa maji baada ya kuteleza na mkondo wa maji kumtupa katika Mto Kanyere uliokuwa umefurika. Mume wa mwanamke hiyo Cornel Sokoni (67) akinusurika.
Inasemekana kuwa tukio hilo lilitokea kutokana na mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha kwa wiki moja katika maeneo ya Mkoa wa Rukwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Kyando amesema kifo hicho kimetokea Februari 27, mwaka huu saa moja na nusu usiku katika Kijiji cha Tatanda wilayani Kalambo.
Sokoni amesema jioni ya siku hiyo, yeye na mkewe walikuwa wanatoka shamba wakienda nyumbani kwao kijiji cha Tatanda huku mvua kubwa ikinyesha.
“Mke wangu alitangulia mie nikimfuata nyuma yake nikiwa nimebeba mzigo wa kuni kichwani, ghafla akateleza na kuanguka kwenye mkondo wa maji ambao ulimtupa ndani ya Mto Kanyere ….Nilijitahidi kadri nilivyoweza kumuokoa lakini sikuweza kwani baada ya kusukumwa na kutupwa ndani ya mto uliokuwa umefurika maji sikuweza kumuona tena,” alieleza.
Kwa mujibu wake, mwili wa marehemu ulionekana siku iliyofuata ukiwa umening'inia kwenye miti umbali wa mita 300 kutoka eneo la tukio baada ya kumtafuta kando ya mto huo.
Winfrida amezikwa juzi kijijini humo.
Kamanda Kyando amewataka wananchi kuwa makini wanap[ovuka mito hasa katika kipindi hiki cha masika kwa kuwa mvua kubwa zinaendelea kunyesha.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin