Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alimwaga machozi mbele ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara wakati wa ibada ya Jumapili.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria ibada ya siku hiyo, alijikuta akibubujikwa na machozi baada ya kupewa nafasi ya kuwasalimia waumini wa kanisa hilo.
Kabla ya kuanza kulia, Makonda alikuwa ametumia muda wake madhabahuni kueleza nia yake ya kuendelea na mapambano ya dawa za kulevya jijini.
Misa ya jana katika Usharika wa Kimara ilikuwa ni mahsusi kwa ajili ya kuombea vyeti vya kuzaliwa, vya masomo na mikataba ya ajira kwa Wakristo wa hapo.
Wakati wa akitoa salamu hizo, Makonda alisema nchi kupitia Dar es Salaam imekuwa ndiyo mlango wa kuingiza na kutoa dawa za kulevya hivyo hatoweza kukaa kimya na kushuhudia watoto na taifa vikiangamia.
“Hizi ni dalili kwamba kazi ninayoifanya katika ulimwengu wa roho inalipa, hakuna aliyemcha Mungu anayeweza kuacha kusimama katika kusudi zuri ambalo Rais wetu ametuelekeza akabaki kupiga kelele hizo ndogondogo.
“Sijui kama unafahamu baba mchungaji wamefikia hatua ya kusema sasa hata mke wangu si raia wa Tanzania…vita hii haipiganwi kienyeji ni lazima uwe umekaa sawasawa,” alisema Makonda.
Alisema historia ya vita vya dawa za kulevya haijawahi kumuacha mtu salama ndani ya Taifa na kwamba hata sasa maswali yamekuwa mengi juu yake.
“Kila aliye jaribu ama alikufa, alifungwa, alipata kila aina ya msukosuko na hatimaye jambo hilo likafanya waovu, wauaji wapate mali kwa njia isiyokuwa halali. Wakapata nguvu na kutengeneza hofu ya kwamba yeyote yule ajaribuye kushughulika nao atashughulikiwa.
“Ndio maana mara kadhaa nimekuwa nikisema ni lazima uwe unamjua Mungu, uwe na uhakika na Mungu unayemwamini na kama huna uhakika usithubutu kuingia kwenye mapambano haya,” alisema.
Aliwabeza wanaoendelea kumjadili na kusema kuwa ukuu wa mkoa si tatizo bali hoja ni namna gani ameitumia nafasi aliyopewa kutekeleza kusudi la Mungu hapa duniani.
“Maswali yamekuwa mengi juu ya njia lakini unapotaka kuwavusha watu kwenda ng’ambo ya pili hakuna mjadala juu ya njia.
“Kuwa mkuu wa mkoa si tatizo, tatizo umeikamilishaje kazi ya Mungu aliyokupa hapa duniani, hapa tuko kwenye vita na vita hii si ya ulimwengu wa mwili bali ni ya ulimwengu wa roho.
“Wananchi wa wamechanganyikiwa, kila wakipita mahala wanaona watoto wanatumia dawa za kulevya na wakiangalia nyuma wanaona wale wauzaji wakubwa hawashikiki, wanatisha, hawajui wapite wapi,”alisema.
Alisema Jiji la Dar es Salaam ndilo lango kuu la uchumi ambapo asilimia 80 ya mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanatoka Dar es Salaam. Hata hivyo limekuwa lango la uchumi mbadala wa kuingizia dawa za kulevya na kuangamiza taifa.
“Rais hawezi kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi sekondari ama kuwakopesha watoto wasome halafu wakaendelea kuvuta bangi ama kutumia dawa za kulevya je, ni mzazi gani mwenye akili timamu atakaye furahia hilo, kiongozi gani mwenye ufahamu wa kimungu anayefurahia hilo?
“Mcha Mungu gani anaweza akakaa kwenye mkoa kama huu akaruhusu madawa yapite halafu watoto wanateketea, mcha Mungu anaweza akaruhusu uovu uendelee kutawala halafu anajiita anamtumikia Mungu?
“Mcha Mungu gani huyo…nikisema mtamjua, sikatai dini yake na wala sitaruhusu akatize katika anga la utawala nililopewa, nimepewa bendera ya Tanzania, nimepewa mamlaka nina ‘operate’ kutoka kwenye mamlaka ya juu sana. Nitasimama hadi mwisho kuhakikisha jina lipitalo majina yote linainuliwa,” alisema Makonda huku akishangiliwa.
Mara kwa mara katika mahubiri yake alikuwa akitoa mifano kwa kutumia baadhi ya maneno kutoka katika kitabu cha Biblia na kushangiliwa na waumini wa usharika huo.
“Vita tuliyonayo ni kazi ya mauti na uzima, kuhakikisha tunamtoa mtoto fulani kwenye makucha ya shatani na hii kazi yesu alishaifanya…ukitaka kujua kaifanya wapi soma.
“Shetani anafitinisha, anachonganisha, anaharibu, anateketeza lakini yesu amekuja kurejesha kilichopotea na ndio kazi tunayoifanya sisi,”alisema.