Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MZEE ANUSURIKA KUFA AKIPAMBANA NA FISI ALIYEVAMIA ZIZI LA MBUZI KISHAPU...TAZAMA PICHA HAPA



Mzee Sylas akionesha mkono uliojeruhiwa na fisi-Picha kwa hisani ya Boniphace Butondo-Kishapu
Fisi akiwa amekufa baada ya kushambuliwa na wananchi

Mwanamme aliyejulikana kwa jina la Sylas Ngeleja(65) mkazi wa kitongoji cha Mwabuli kijiji cha Mwamadulu kata ya Lagana wilayani Kishapu mkoani Shinyanga amenusurika kufa baada ya kushambuliwa na fisi aliyevamia zizi la mbuzi. 

Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde1 blog kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi Machi 04,2017 majira ya saa nane usiku. 

Wamesema kundi la fisi lilizunguka zizi la mbuzi la mzee Sylas Ngeleja kisha fisi mmoja kuanza kula mbuzi ndipo mzee huyo alipoamua kuingia zizini na kuanza kupambana na fisi huyo ambaye tayari alikuwa ameua mbuzi mmoja. 

Akisimulia kuhusu tukio hilo Diwani wa kata ya Lagana Boniphace Butondo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu amesema baada ya fisi huyo kuingia zizini ndipo mzee huyo alipoamua kuanza kupambana naye. 

“Majirani walijitokeza na kukuta kundi la fisi wakiwa wamezunguka zizi huku mmoja akiwa ndani ya zizi ndipo wakatoa msaada kwa mzee huyo na fisi huyo tayari alikuwa amemjeruhi mzee huyo mkono wa kushoto na kumsababishia majeraha kisha kumkimbiza katika zahanati ya Lagana kwa ajili ya matibabu”,ameongeza Butondo. 

Amesema wananchi walifanikiwa kumuua fisi huyo na kuongeza kuwa hivi sasa kuna tishio la fisi katika kata ya Lagana ambapo fisi wamekuwa wakizagaa kuanzia saa 12 jioni. 

“Nafanya mawasiliano na mkurugenzi wa halmashauri ya Kishapu ili tuangalie namna ya kumaliza tatizo hili kwani kata ya Lagana imezungukwa na vilima ambapo kuna mapango ya fisi”,amesema Butondo. 

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalam wilaya ya Kishapu ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Nyabaganga Talaba ameiambia Malunde1 blog kuwa bado hajapata taarifa kuhusu tukio hilo na kwamba atachukua hatua kama tukio hilo lipo. 

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com