Maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani “World TB Day” mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika machimbo ya dhahabu ya Nyangarata kata ya Lunguya halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama.
Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yamefanyika Machi 24,2017 katika kitongoji cha Nyangarata,kijiji cha Kalole kata ya Lunguya ambapo kuna shughuli za uchimbaji wa madini.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na timu ya afya mkoa wa Shinyanga na za wilaya kwa ushirikiano mkubwa wa shirika lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu,Geita,Mara,Mwanza na Tanga.
AGPAHI pia ni wadau wa muda mrefu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Tuungane Kutokomeza Kifua Kikuu’ alikuwa mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga.
Awali akisoma risala katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani,Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele alisema kutokana na ushirikiano wanaopata kutoka serikalini wamepanua zaidi huduma za ushauri nasaha na upimaji VVU,tiba na matunzo ya watu wanaoishi na VVU na uchunguzi wa kifua kikuu katika maeneo ya migodi na maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Alisema hivi sasa shirika hilo linatekeleza mradi wa kifua kikuu migodini tangu mwezi Desemba 2016 wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu kifua kikuu kwa wachimbaji pamoja na wananchi wanaoishi maeneo hayo ili waweze kuchukua hatua za haraka kujikinga na kupata tiba sahihi ya kifua kikuu.
“Katika kipindi cha miezi minne ya mradi huu,jumla ya watu 2637 walifanyiwa uchunguzi wa kifua kikuu wakiwemo wanaoendelea kuchimba na walioacha kuchimba na familia zao,kati yao 364 walihisiwa kuwa na kifua kikuu",alieleza Dkt. Mabelele.
Alibainisha kuwa kati ya watu hao 364, 345 kati yao walipelekwa kwenye uchunguzi ambapo 16 wakiwemo watoto watatu walibainika kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu na hivyo kuanzishiwa matibabu.
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Nuru Mpuya alisema mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya nne kitaifa kwa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu ambapo mikoa inayoongoza ni Dar es salaam,Mbeya na Mwanza.
Dkt. Mpuya alizitaja sababu zinazochangia maambukizi hayo kuwa ni wananchi kuchelewa kufika katika vituo vya tiba,imani potofu kwa wananchi kukimbilia kwa waganga wa jadi wakiamini kuwa wamerogwa na uhaba wa vifaa vya uchunguzi.
Aidha Dkt. Mpuya alilipongeza shirika la AGPAHI kwa kuisaidia serikali vifaa vya kuchukulia sampuli za makohozi,hadubini za kisasa katika vituo vya afya ikiwemo cha Lunguya ambacho kimepewa mashine ya uchunguzi wa kifua kikuu iitwayo “Gene Xpert”.
Naye mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ,mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliwataka wananchi kuachana na imani potofu za kuamini waganga wa jadi na badala yake wanapoona dalili za ugonjwa wa kifua kikuu wafike katika vituo vya afya kupima afya zao kisha kuanza huduma ya matibabu.
Mkuu huyo wa wilaya alitahadharisha kuwa huduma za kupima kifua kikuu na matibabu zinatolewa bure hivyo kuwanyooshea kidole wale watakaobainika kuomba fedha kwa ajili ya huduma hiyo ambapo alitoa agizo la maduka binafsi ya dawa za binadamu kuacha mara moja kuuza dawa zinazotibu ugonjwa wa kifua kikuu.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika wakati wa maadhimisho hayo katika machimbo ya Nyangarata ni huduma ya kupima VVU,kufanya uchunguzi wa kifua kikuu,tohara kwa wanaume na kuandikisha watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa ajili ya vyeti vya kuzaliwa lakini pia shirika la AGPAHI kukabidhi baiskeli kwa watoa huduma ngazi ya jamii wanaofanya kazi ya uchunguzi wa kifua kikuu migodini.
Angalia hapa matukio katika picha yaliyojiri wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani katika mkoa wa Shinyanga kwenye machimbo ya Nyangarata wilayani Kahama.
Katikati ni mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Msalala Simon Berege akimwongoza Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya siku ya Kifua kikuu duniani mkoa wa Shinyanga kwenda kukagua mabanda yaliyokuwa yanatoa huduma za kupima VVU,uchunguzi wa kifua kikuu,tohara na huduma zingine za afya sambamba na zoezi la kuandikisha watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu (mwenye suti nyeusi) na Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa Dkt. Nkingwa Mabelele(kulia) wakisikiliza maelezo ya wataalamu wa afya katika banda la kupimia VVU
Ndani ya banda la uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu-Wataalamu wa afya wakitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu
Zoezi la tohara kwa wanaume linaendelea-Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akiwa katika banda la kutolea huduma ya tohara kwa wanaume bure.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akiwa katika banda la kutolea huduma mbalimbali za afya ikiwemo huduma ya mama na mtoto
Kushoto ni mratibu wa huduma za maabara mkoa wa Shinyanga Muhdin Hamza akimweleza jambo mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akizungumza na wataalamu wa afya kutoka kituo cha afya Lunguya waliokuwa wanaendesha zoezi la kuandikisha watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili wapatiwe vyeti vya kuzaliwa
Wakazi wa Nyangarata wakiwa katika mabanda yaliyokuwa yanatoa huduma za upimaji wa VVU na uchunguzi wa kifua kikuu
Zoezi la kuandikisha watoto wenye miaka chini ya mitano ili wapate vyeti vya kuzaliwa likiendelea. Kitongoji cha Nyangarata ambapo kuna machimbo ya madini ya dhahabu kimepewa upendeleo wa kuwekewa kituo cha kuandikisha watoto badala ya kwenda kwenye ofisi ya kata ya Lunguya au vituo vya afya vilivyopo katika kata hiyo
Watoa huduma wakitoa maelezo kwa wakazi wa Nyangarata kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu kwenye banda lililokuwa linatoa huduma za uchunguzi wa kifua kikuu
Mchimbaji mdogo wa madini akichukuliwa damu kwa ajili ya kupima VVU
Diwani wa kata ya Lunguya Benedict Mussa akiwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo ambapo alisema eneo la Machimbo ya Nyangarata ni miongoni mwa maeneo ambayo yana watu wengi wenye ugonjwa wa kifua kikuu ndiyo maana maadhimisho ya siku ya kifua kikuu yamefanyika hapo
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele akisoma risala fupi kuhusu mradi wa kifua kikuu migodini ulioanzishwa na shirika la AGPAHI mwaka 2016 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu kifua kikuu kwa wachimbaji wa madini na wananchi wanaoishi maeneo hayo. Mradi huo unafadhiliwa na shirika la ADPP la Msumbiji.
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele alisema shirika hilo limekuwa likisaidia katika kutoa mafunzo kuhusu huduma za kifua kikuu na UKIMWI kwa watumishi wa afya na kutoa elimu kwa umma kwa njia ya radio na kufundisha wahudumu katika ngazi ya jamii ili waweze kutoa huduma katika maeneo ya migodi
Wananchi wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Dkt. Mabele alieleza kuwa shirika la AGPAHI kupitia wafadhili wake limeweza kununua na kusambaza vitendea kazi kama vile baiskeli na vifaa vya kuchukulia sampuli za makohozi, hadubini 8 za kisasa kwa ajili ya vituo vya afya vya Bugarama,Lunguya,Chela,Segese,Chambo,Ushetu,Nindo na Tinde.
Dkt. Mabelele aliongeza kuwa shirika la AGPAHI limenunua mashine moja ya uchunguzi wa kifua kikuu 'Gene Xpert' yenye uwezo wa kupima na kugundua uwepo wa kifua kikuu na kutambua usugu dhidi ya dawa za kifua kikuu katika kituo cha afya Lunguya katika halmashauri ya wilaya ya Msalala
Maafisa kutoka AGPAHI wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea eneo la tukio
Mkazi wa Nyangarata Robert Mayinja akitoa ushuhuda baada ya kupona ugonjwa wa kifua kikuu ambapo aliwataka wananchi kufika katika vituo vya afya kupima afya zao pale wanapoona kuna dalili za ugonjwa wa kifua kikuu na kuhakikisha wanapata tiba kwani ugonjwa wa kifua kikuu unatibika
Meneja wa AGPAHI kanda ya ziwa, Dkt. Nkingwa Mabelele akikabidhi baiskeli kwa mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu ili awakabidhi watoa huduma ngazi ya jamii wanaofanya kazi ya uchunguzi wa kifua kikuu katika maeneo ya migodi halmashauri ya Msalala
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimkabidhi baiskeli mmoja wa watoa huduma hao.AGAPHI imetoa baiskeli tatu ikiwa ni nyongeza ya baiskeli zingine 12 zilizokwisha tolewa awali kupitia mradi wa kifua kikuu migodini
Mtoa huduma ngazi ya jamii anayefanya kazi ya uchunguzi wa kifua kikuu akiendesha baiskeli yake baada ya kukabidhiwa
Kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Nuru Mpuya akizungumza katika maadhimisho hayo ambapo alilipongeza shirika la AGPAHI kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu
Meza kuu wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Wakazi wa Nyangarata wakiwa katika mabanda ya huduma ya upimaji wa VVU na uchunguzi wa kifua kikuu
Kaimu katiba Tawala mkoa wa Shinyanga Mohammed Nchira akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ambapo alisema jitihada zaidi zinatakiwa ili kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu mkoani Shinyanga huku akiwataka wananchi kufika katika vituo vya afya kupima afya zao na kuanza huduma za matibabu pale wanapobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani mkoa wa Shinyanga ambapo aliwataka wananchi kuepuka kutumia muda mwingi kwa waganga wa kienyeji kwani hawawezi kutibu ugonjwa wakifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu alisema vipimo vya kifua kikuu vinatolewa bure hivyo kuwataka wananchi kuwafichua wanaotoza pesa kwa ajili ya huduma ya vipimo na hata dawa za ugonjwa wa kifua kikuu
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu alitumia fursa hiyo pia kulipongeza shirika la AGPAHI kwa kazi nzuri linalozifanya mkoani Shinyanga hususani katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI na ugonjwa wa kifua kikuu huku akiyaomba mashirika mengine kujitokeza kuwasaidia wananchi wa mkoa huo
Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu pia akatumia fursa hiyo kuwahamasisha wakazi wa Nyangarata kuimarisha amani katika eneo hilo ambalo lilianza kusifika kwa matukio ya kihalifu
Mkurugenzi wa halmashauri ya Msalala mheshimiwa Simon Berege akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu duniani
Mkazi wa kitongoji cha Nyangarata akipokea zawadi ya tisheti baada kujibu maswali yanayohusu ugonjwa wa kifua kikuu
Mkazi wa kitongoji cha Nyangarata akijibu maswali kuhusu jinsi ugonjwa wa kifua kikuu unavyoambukizwa na jinsi ya kupata tiba
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin