Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AKERWA NA MKANDARASI MVIVU MTWARA

Rais John Magufuli ameigiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumsimamia kwa karibu mkandarasi aliyeshinda zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mtwara, Tandahimba, Newala hadi Masasi kwa kuwa ana historia ya kutofanya vizuri.

Kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa kilometa 50 kati ya 210 za barabara hiyo ni DOTT Services LTD kutoka nchini Uganda inayodaiwa kuwa ilichelewesha kazi ilipokuwa inajenga barabara ya Same hadi Mkambala wakati huo Magufuli akiwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi.

"Nina mashaka sana na huyu mkandarasi mliyempa kazi ya ujenzi wa hii barabara...namjua huyu alitusumbua, alijenga barabara ya Same hadi Mkambala alicheleweshakazi," amesema Rais Magufuli.

Alisema kushinda zabuni kwa kuweka kiasi kidogo kuliko wote si sababu pekee ya kuifanya kampuni kupata kazi kwani anaweza kutaja kiasi kidogo lakini akachelewesha kazi na hivyo kuongeza gharama maradufu.

"Ninaposema haya najua mnanielewa...kama ningekuwa ni mimi nisingempa kazi huyu maana namjua, nimeshangaa kumkuta huku tena...sasa hiyo kazi isimamiwe kwa karibu kuhakikisha hatusumbui,"amesema Rais Magufuli.

Amesema kuwa kwa kuwa wameshampa kazi ni wajibu kwa wizara na vitengo vyake vyote akiwemo Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Mtwara kuhakikisha wanamsimamia kwa karibu ili kazi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.

"Hakikisheni kazi hii inafanyika vizuri, ikitokea yale ya kule mimi nitajua nini cha kufanya na ninyi maana mnanijua...kwa kuwa nitakuja kuweka jiwe la msingi basi mwambieni hizi ni salamu zake kutoka kwangu,"amesema Rais Magufuli.

Kampuni hiyo tayari imeshasaini Mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kutoka mjini Mtwara hadi Mnivata umbali wa kilometa 50 kwa thamani ya Sh bilioni 89.6 ambapo Mkataba huo ulisainiwa Januari 19, mwaka huu, huku kazi ya ujenzi ikitarajiwa kuchukua miezi 21 pamoja na muda wa maandalizi.

Aidha Kampuni ya Kyong Dong Engineering Co LTD kutoka Korea ikishirikiana na Core Consulting PLC kutoka Ethiopia na kampuni ya Mhandisi Consultancy LTD ya Tanzania ndio zilizoshinda zabuni ya ushauri wakati wa ujenzi huo kwa gharama ya Sh bilioni 2.9 na tayari Mkataba umeshasainiwa.

Raisi Magufuli yupo mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa gati, pia alifungua jengo la Benki Kuu (BoT0), Kanda ya Kusini, Kituo cha Biashara cha Benki ya NMB na kufungua nyumba za makazi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Leo Rais atatembelea Kiwanda cha Saruji cha Dangote na baadaye kuhutubia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com